Na Joseph Ngilisho,Arusha
WAZIRI wa Fedha na Mipango dkt, Mwigulu Nchemba ameitaka benki kuu Tanzania [BOT], kuhakikisha inasimamia ipasavyo kanuni ,taratibu na sheria katika kuhakikisha benki zote nchini zinafanya kazi zao kwa kuzingatia weledi katika kuwahudunia wananchi.
Waziri Nchemba,aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizindua tawi jipya la benki ya Mwanga Hakika jijini Arusha na kuitaka benki hiyo kujiendesha kwa kutoa huduma nzuri na bora kwa wateja wake .
Aliwashauri wateja waliokopa katika taasisi za fedha kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha wengine nao kukopa kwa kuwa benki zimesaidia ukuaji wa pato la taifa kwa mtu mmoja mmoja.
Mbali na hilo Nchemba ameitaka BoT kuimarisha nidhamu katika soko kwa taasisi za fedha kuongeza uwazi na kutumia sera za kifedha kupitia changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika mfumo wetu wa kibenki kwa wateja wao.
Aidha Mwigulu alikemea baadhi ya wafanyakazi wa benki wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu taasisi za fedha kwa kutoa mkopo na baadaye fedha hizo kwenda kutumika kinyume na malengo yaliyoombewa na kusababisha mkopo huo kutolipika .
‘’ Watu wanaomba fedha kwenye taasisi za kifedha lakini hawana malengo nayo ,ninawaonya maafisa wote wa benki kuhakikisha kuwa kila mkopaji awe na lengo linaloeleweka ili aweze kurejesha kwa wakati “alisisitiza dkt Nchemba
Waziri ,huyo aliwataka wananchi kuwa na nidhamu ya mikopo kwani watu wengi wamekuwa wakichukua mikopo hawajui wanaifanyia nini kwa kuwa hawajajiandaa nashughuli watakayoifanyia mikopo hiyo.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Mwanga hakika benki, Ridhiwani Mringo,alisema kuwa benki hiyo imejipambanua katika kuwahudumia wateja wengi zaidi ambapo itatoa faida kwa wenye hisa na wateja wengine wa benki hiyo ,.
Mringo, alisema kuwa benki zimesaidia ukuwaji wa uchumi na hivyo kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Awali mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo ,Jagjit Singh , alisema benki hiyo ilianza mwaka 1998 ikiwa ni benki ya kijamii na mwaka 2020 ilikuwa ni benki ya Microphinance na kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa ni benki ya biashara.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba lengo ni kuifanya iwe ya kimataifa zaidi kutoka nchini hadi itoe huduma zake ukanda wa Afrika mashariki lengo ni kuhudumia watu wengi zaidi na kwamba benki hiyo inatoa riba ya asilimia 12% kwa atake weka akiba .
Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Felisian Mtehengerwa aliwahakikishia wawekezaji wa benki hiyo kuwa Arusha ni mji salama wa kibiashara, unaochochewa na sekta ya utalii,hivyo aliwasihi kuhakikisha wanafanya uwekezaji mkubwa na utoaji wa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara.
Ends....
0 Comments