Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
BARAZA la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa miezi sita kwa wamiliki wa bar,kumbi za starehe na baadhi ya makanisa yanayoendesha shughuli zake kwa kelele chafuzi hasa nyakati za usiku ,kusitisha mara moja kabla baraza hilo halijachukua hatua kali ikiwemo kuyafungia.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, dkt Samwel Gwamaka wakati alipotembelea moja ya kanisa lililopo mtaa wa Sana ,kata ya Moivo wilayani Arumeru kwa lengo la kulifunga baada ya kuwepo malalamiko ya muda mrefu kuhusu kelele chafuzi.
"Tumepata malalamiko ya muda mrefu ya takribani miaka mitatu kwa kanisa la mchungaji Masawe wa kanisa la Ebenezer ambapo majirani wamekuwa wakilalamikia kelele zinazotokana na mikesha nyakati za usiku"
Alisema Mchungaji huyo mbali na maonyo kadhaa ya NEMC kanda ya Kaskazini aliwahi kufikishwa mahakamani na kutizwa faini ya sh,milioni mbili lakini hakulipa amekuwa akikaidi maelekezo yote yanayotolewa.
"Leo tumekuja hapa kujiridhisha na lengo letu ni kufunga hii huduma ya kanisa na sheria inaturuhusu ofisi yetu ya kanda iliwahi kufika hapa na kupima kiwango cha sauti na kujiridhisha kwamba kiwango cha sauti kimezidi"
Licha ya mmiliki wa kanisa hilo kuwa na usajiri,lakini limejengwa kwenye makazi ya watu kinyume cha sheria na halikupaswa kuwepo hapo kwa sababu makazi ya watu yana watoto ,wagonjwa,wazee na nyakati za usiku watu wanapaswa kupumzika na sio kubughudhiwa.
"Tumemuelimisha lazima abadilishe matumizi ya eneo hili ndani ya miezi sita na tukisikia malalamiko yoyote ya kelele, kifungu cha 151 cha sheria ya mazingira kitatumika kufunga kanisa hili na hii sio kwa kanisa hili tu ni kwa nchi nzima ".
Naye Baraka Shange mwenyekiti wa kitongoji cha Sana alisema kuwa amekuwa akiletewa malalamiko ya muda mrefu kuhusu kanisa hili kupiga kelele chafuzi na nilikuwa natoa ushauri kwa kiongozi wa kanisa hili lakini alikuwa akipunguza kwa muda na baadaye kuendelea na kelele.
Kwa upande wake mchungaji,Selestine Masawe aliishukuru NEMC kwa kumpatia maelekezo ambayo aliahidi kuyafanyia kazi ili kukaa vema na majirani wanaomzunguka na kufuata sheria za Mazingira.
Ends...
0 Comments