GAMBO AMWAGA MBOGA,MBELE YA WAZIRI MKUU MSTAAFU PINDA..MWENYEKITI CCM AMTAKA AACHE UTOTO'usiingize majungu na utoto hapa'


Na Joseph Ngilisho Arusha 

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ameibua tuhuma zingine dhidi ya viongozi wa CCM na Serikali Mkoa wa Arusha akidai kuwa wanampiga vita katika kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi waliomchagua.


 Mbali na hilo Gambo aliwaomba viongozi wa ngazi za juu ndani ya chama hicho kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya viongozi hao wa CCM Mkoa wa Arusha akidai kuwa wanahatarisha chama kuelekea chaguzi zijazo ikiwemo wa Serikali za Mitaa mwakani.


Gambo alitoa tuhuma hizo mbele ya Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda kwenye uchaguzi wa kumpata mjumbe wa NEC Taifa uliofanyika leo Aprili 5, 2023 mkoani Arusha.


Katika uchaguzi huo, Namelok Sokoine amefanikiwa kushinda kwa kura 39 akiwabwaga wenzake tisa akiwemo Daniel Palangyo aliyekuwa anatetea kiti chake lakini ameambulia kura tano.


"Awali, tulikuwa tunapigana na vyama vya upinzani lakini leo niwaambie wazi, tunapigana vita wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama nikiwemo mimi. Nimekuwa nikipingwa kila ninachofanya kwa wananchi na wahusika wakuu ni viongozi wa CCM mkoa na Serikali ya mkoa," amesema Gambo na kuongeza...


"Niombe viongozi wakuu wa chama, kuwa Kamati Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha inahitaji kumulikwa kwa jicho la tatu ili chama kiwe salama maana wameungana kunipiga vita, kisa natekeleza wajibu wangu. Leo niwaambie kuwa nitaendelea kupambana kwa maslahi ya chama hata nikibaki peke yangu, hivyo waendelee kusubiri uchaguzi ujao," amesema Gambo.

Gambo amesema kuwa hana tatizo na viongozi wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini kwani wamekuwa wakishirikiana kwa kila jambo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM  Mkoa wa Arusha, Zelothe Steven alisema kuwa lengo la mkutano huo ulikuwa uchaguzi hivyo usiingizwe majungu na utoto bali wajikite katika kumpongeza Namelok aliyeshinda.


"Arusha ina watu wakomavu katika siasa hakuna utoto hapa na haturudi nyuma katika kutetea maslahi ya chama hivyo kama kuna mtu ana hoja alete katika mahali husika," amesema.


Aidha mbali na tuhuma hizo, hivi karibuni Gambo aliibua tuhuma dhidi ya viongozi wa CCM akidai kufanyiwa majaribio ya kuuawa ikiwemo kutegwa kwa sumu lakini pia kuvamiwa nyumbani kwake na watu aliowatambua ni wa ndani ya chama chake.

Post a Comment

0 Comments