Na Joseph Ngilisho Arusha
Wakazi wa eneo la Tanganyika pekazi jirani na kambi ya jeshi la wananchi Tanzania JWTZ, Katika kata ya Moshono jijini Arusha, huenda wakaondokana na adha ya muda mrefu ya kuzingira na maji ya mvua wakiwa wamelala mara baada ya Mkuu wa wilaya ya Arusha Felisian Mtehengerwa,kutembelea eneo hilo na kumwagiza wakala wa barabara Tanroads Mkoa wa Arusha, kurekebisha mara moja mfumo wa mikondo ya maji ya mvua yanayoingia na kuathiri makazi ya wananchi .
Mtehengerwa ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea na kujionea athari inayotokana na maji ya mvua, ambapo kwa muda mrefu wananchi hao wamekuwa wakilia na kulilaumu jeshi la wananchi Tanzania [JWTZ] kambi ya Tanganyika pekazi,kwa kuweka ukuta na tuta na kuzuia maji kupita kwenye mkondo wake na kuingia kwenye nyumba zao.
Mkuu huyo wa wilaya alishauri mikondo ya maji itazamwe upya kupitia wataalamu wa Tanroads ili kupata jibu sahii litakaloondoa malalamiko ya wananchi.
Hata hivyo mkuu huyo aliwatupia lawama wananchi wanaojenga nyumba kiholela bila kufuata utaratibu ,jambo linalosababisha kuziba kwa mikondo ya maji na kupelekea maji kukosa mwelekeo na kuingia kwenye makazi yao.
Mmoja ya wakazi wa eneo hilo Mosses Kivuyo,alisema kuwa awali walikuwa wakiishi na jeshi hilo bila kuwa ma mgogoro wowote ila wanasikitika mara baada ya jeshi hilo kujenga ukuta maji yalikosa mwelekeo na kuhamia kwenye makazi yao.
Hata hivyo alishukuru ujio wa mkuu wa wilaya na kueleza kuwa utatoa ufumbuzi baada ya kutoa maelekezo kwa Tanroad kufuatilie na kutoa tathimini namna ya kuhamisha mkondo wa maji ili yasiathiri wananchi.
Kwa upande wake mhandisi , Sunday Boaz kutoka kitengo cha Mipango, Tanroads alisema maelekezo ya Mkuu wa wilaya wameyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuondoa adha hiyo kwa wananchi.
Hata hivyo alisema changamoto hiyo imetokana na wananchi kujenga nyumba kwenye mikondo ya asili ya maji na kusababisha maji kukosa mwelekeo na kujaa kwenye makazi yao.
"Tutakuja kama timu ya Tanroads na kuangalia namna ya kuyachepusha maji ili yasielekee kwenye makazi ya watu, lakini kama unavyofahamu maji hayawezi kupanda mlima vinginevyo tutawashauri wananchi wabomoe kuta zao ili kuyapa njia maji yaweze kupita"
Diwani wa kata ya Moshono Miriam Kisawike alisema changamoto ya maji ya mvua kuingia kwenye nyumba za wananchi wa eneo la Tanganyika pekazi ni la muda mrefu hivyo ujio wa dc unaweza kutoa unafuu kwa wananchi hao kuondoka na adha hiyo.
0 Comments