Na Joseph Ngilisho ,Arusha
Mkuu wa wilaya ya ARUSHA Felisian Mtehengerwa amemtaka mbunge wa Arusha kuacha siasa za maji Taka na utoto kwa kutaka huruma ya wananchi kutuhumu viongozi kwa ufisadi wakati yeye ni sehemu ya viongozi wanaosimamia utekelezaji wa mipango ya jiji la Arusha.
Akiongea na waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wake kama mkuu wa wilaya kuhusiana na tuhuma zilizotolewa na mbunge Gambo bungeni, akielezea ubadhilifu wa fedha za umma katika halmashauri ya jiji la Arusha na serikali kuu, alisema mbunge hajui wajibu wake na anaendesha siasa za kitoto .
"Nadhani hapa kuna tatizo watu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia halmashauri ni madiwani na mbunge mwenyewe lakini hawajui dhamana yao, kama waliona kuna mambo hayaendi vizuri wangekuwa wakwanza kuzuia na kuchukua hatua za awali ila kinachofanyika hapa ni siasa za kitoto"
Alisema anachokifanya Gambo ni kutafuta njia ya kutokea na kusaka umaarufu usio na tija ,na watu wenye upeo mkubwa na uelewa wanaweza kumhoji,alikuwa wapi wakati mambo hayo yakitokea ama na yeye ni sehemu ya mpango huo.
"Kama haya anayoyasema yapo, watu ambao wamepewa mamlaka ya kusimamia halmashauri ni pamoja na Mbunge na madiwani na kama hawakutimiza wajibu wao basi hawatoshi "
'Sisi kama wilaya tunawajibu wa kuingilia pale tunapoona akili za halmashauri zimefikia ukomo na mambo hayaendi, nilipoingia madarakani nilizungukia miradi yote na kuwaita madiwani wote na kutoa maelekezo "
Alisisitiza kuwa hayo mambo yanayotajwa sasa na mbunge yamefanyika mwaka mmoja au miwili iliyopita na mengine yapo mahakamani na mamlaka zingine zinaendelea na uchunguzi...
Hivi karibuni Gambo akiwa bungeni dodoma akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ya mwaka wa fedha 2023/24 alitaja mambo kadhaa ya ufisadi katika jiji la Arusha huku akidai changamoto kubwa ni ubadhilifu na usimamizi mbovu wa fedha za halmashauri.
Alitolea mfano baadhi ya tuhuma ukiwemo ujenzi wa jengo la utawala lenye urefu wa orofa sita katika jiji la Arusha,ambapo alisema halmashauri imetafuta fundi mjenzi (rafiki yao) bila kutangaza tenda, taratibu za manunuzi hazikufuatwa na kumpatia kiasi cha fedha sh, milioni 199.7 kinyume na utaratibu.
Pia alidai halmashauri hiyo ilinunua vifaa vya sh, milioni 132 ambavyo havikufika eneo la mradi.
"Pia waliongeza ziada ya nondo kiasi cha tani 6.48 zenye thamani ya sh,milioni 17 pia waliongeza malipo ya sh, milioni 21 kwa fundi yanayotokana na uzembe wa wataalamu wetu"
"Kumekuwepo na lisiti feki za EFD zenye thamani ya sh, milioni 699.9 ambapo fedha hizo hazijulikani zimefanya nini"
"Mbunge akizungumza wanasema kuwa anataka ugomvi, sasa kipi bora, bado kuna dokezo tena la Sh12 milioni kwa mtu mwingine, nawaambia siwezi kunyamaza, nimejitoa kafara kusema kuwa watumishi wa Serikali za mitaa wanashirikiana na wale wa Serikali kuu kula fedha,” alisema Gambo.
Mbunge huyo ambaye amekuwa na migogoro ya ndani na viongozi wa jimbo lake, alisema kuna fedha nyingi zimeliwa kwa kigezo cha kuwajengea machinga ikiwemo Sh, milioni 86 ambazo zilipelekwa kujenga soko la Machinga, lakini muda mfupi lilibomolewa kwa maana limejengwa eneo ambalo si rafiki.
Tuhuma kama hizo, aliziibua Mei 24 mwaka jana, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Arusha ambapo aliwatuhumu viongozi wa CCM na Serikali akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Jiji la Arusha, Dk John Pima kwa kula fedha za jiji.
Kutokana na tuhuma hizo za Gambo hadi sasa Dk Pima na maofisa wengine wa jiji wanaendelea na kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na leo watakuwa wanajitetea mahamani hapo.
Ends...
0 Comments