WAZIRI KIRUSWA ACHARUKA AIPA WIKI TATU RUWASA ITOE MAJI LONGIDO

 


Na Joseph Ngilisho,Longido


Naibu Waziri wa Madini,Dkt Stephen Kiruswa amemwagiza Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini {RUWASA} Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kuhakikisha ndani ya wiki tatu maji yanapatikana katika kata ya Olmolok wilayani humo kwa kuwa serikali ilishatoa shilingi milioni 903 kwa ajili ya mradi huo na mradi ulipaswa kukamilika juni mwaka jana.


Dkt Kiruswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido alionyesha kusikitishwa na hali hiyo pale alipotembelea kata hiyo na kupokelewa na akina mama wakibeba ndoo tupu za maji huku wakilalamika kukosekana kwa maji na wanapouliza kwa viongozi wa mradi huo hutishiwa kukamatwa na kufunguliwa mashitaka na Kiruswa alimwagiza Mkuu wa kituo kushughulika na wale wenye kutishia wananchi.



Alisema serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ilitenga bajeti ya shilingi milioni 903 kwa ajili ya mradi wa maji katika kata hiyo na kata za jirani lakini hadi sasa mkandarasi amelipwa shilingi milioni 300 na hajui kwa nini pesa zilizobaki zinafanya nini na hajui kwa nini mradi huo haujakamilika kwani ulipaswa kukamilika juni mwaka jana.


Waziri alisema kutokana sitofahamu hiyo alimwagiza Meneja wa RUWASA longido Petro Nyerere ndani ya wiki tatu maji yawe yamepatikana katika kata hiyo na afuatilie pesa zilikokwama ili Mkandarasi wa Mradi huo apewe fedha zake aweze kukamilisha mradi huo.


Naye Meneja wa RUWASA,Petro Nyerere alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kumetokana na changamoto nyingi kwa Mkandarasi ikiwemo usafiri wa kusafirisha vifaa kutoka Makao makuu ya wilaya na kuchelewa kwa fedha kumfikia Mkandarasi kwa wakati.


Nyerere alisema baada ya Mbunge Kiruswa kukubali kutoa usafiri wake kusafirisha vifaa vya ujenzi na kusimamia malipo ya Mkandarasi kazi ya mradi huo huenda ikakamilikaa ndani ya muda waliopewa kwani hakutakuwa na kisingizo na kuwataka wananchi kumpa ushirikiano Mkandarasi.


Naye Mkazi wa kata hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Neema Lee alisema kuwa akina mama hutembea umbali wa zaidi ya km 6 usiku wa manane kusaka maji na hukutana na changamaoto nyingi njiani ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ngono zembe na wanaume na kujikutaka kupata mimba zisizotarajiwa na wengi kupata ugonjwa wa Ukimwi hivyo walimshukuru Mbunge wa kuliona hilo na kusimamia mradi wa maji utekelezeke.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Olmolk,Parit Laizer,Diwani wa kata ya Olmolk Loomoni Mollel na Mwenyekiti wa CCM Kata Raphael Simoni wote kwa nyakati tofauti walimtupia lawama Mkandarasi na Meneja wa RUWASA kwa kushindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati.


Walisema akina mama wa kata hiyo wanahangaika huko na kule kusaka maji wakati serikali imetenga pesa kwa ajili ya mradi huo lakini hawajui ni kitu gani kimezuia kukamilika kwa maradi huo hivyo walimwomba Mbunge kuhangaika na Mkandarasi maana kwao ameonyesha dharau pindi anapoulizwa kukwama kwa mradi huo.


‘’Mheshimiwa hali ni mbaya sana hapa akina mama wanaamuka usiku mnene kusaka maji usiku una mambo mengi kwani wengine wanafanyiwa vitendo vya hovyo na wahuni na wengine wanapoteza masiha na wanyama wakali tunaomba msaada juu ya kukamilika kwa mradi huu’’alisema Saimon


Wakati huo huo Mbunge Kiruswa amewazawadia Cherehani 10 akina mama wa Kata Olmolk zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3 lengo ni kutaka akina mama hao kujikwamua kiuchumi katika maisha yao ya kila siku.


Ends..

Post a Comment

0 Comments