WAANDISHI WA HABARI WALIOATHIRIKA NA MGOGORO WA ARDHI NGORONGORO WAKUTANA NA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA


Na Joseph Ngilisho, Arusha 

Tume ya haki za binaadamu na Utawala bora  nchini(THBUB),imekutana na waandishi wa habari mkoani Arusha, ambao wamewahi kuathirika na mgogoro wa ardhi wa Loliondo na Ngorongoro.


Tume hiyo imeamua kukutana na wanahabari waliowahi kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu, baada ya kupokea wito kutoka wa asasi za kutetea haki za binaadamu mkoa Arusha.

 

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema walikuwa Loliondo na Ngorongoro kuwasikiliza wananchi na wakapata maombi kuja kuwasikiliza na wanahabari ambao kwa namna moja ama nyingine wameathirika na matukio ya Loliondo na Ngorongoro.

 


Lilian Oddo Mwandishi wa Habri wa Leo TV akizungumza mbele ya Tume ya Haki za Binadamu Nchini kuhusu madhila aliyokutana nayo katika utendaji wa kazi

 


Wakizungumza na tume hiyo, wanahabari  waliowahi kukumbwa na madhila uya ukiukwaji wa haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao Julius Msagati (star Tv), Lilian Oddo( Leo Tv) na Profit Mmanga( Wasafi TV) waliieleza tume hiyo kuwa waliwahi kukamatwa na kuwekwa rumande kutokana na kuandika habari za Ngorongoro.


Msagati alisema mnamo mwezi june mwaka jana, akiwa na waandishi wengine, walialikwa na wananchi katika kijiji cha Nainokanoka ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na baada ya mkutano na wananchi walikamatwa na askari wa mamlaka hiyo.


"Tulikamatwa tukapekuliwa kwa zaidi ya masaa matano bila kuelezwa makosa yetu na baada ya mlalamiko kufika ngazi mbali mbali tuliachiwa saa nne usiku kutoka Ngorongoro"alisema

 



 

Mwanahabari Oddo na Mmanga walieleza kukaa rumande wa kituo kikuu cha polisi Arusha, kitengo cha Utalii kwa siku mbili baada ya kukamatwa kutokana na kuandika habari za wananchi kuhusiana na zoezi la kuhamishwa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwenda Msomera.


"Tulikamatwa maeneo tofauti kama wahalifu na kupelekwa polisi na tuliandika maelezo, lakini baada ya siku mbili tulitolewa na Waziri wa mambo ya ndani, Hamad Masauni ambaye alikuwa kwenye ziara Arusha hasa baada ya malalamiko ya wanahabari"alisema


Alisema licha ya kuachiwa Runinga yake ya mtandao aliyokuwa anaisimamia ya Leo Tv iliondolewa mtandaoni.


Mwandishi mwandamizi wa star tv, Angelo Mwoleka alisema wakati wa zoezi la kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro na kumegwa eneo la loliondo kuanzishwa pori la akiba Pololeti kumekuwepo na ukiukwaji wa haki za binaadamu.


Mwoleka alisema wanahabari walikuwa wakipokea simu za vitisho kutoandika habari za wananchi na badala yake waandishi maalum walipewa jukumu la kuandika habari za upande mmoja tu na hivyo kuwanyima haki watanzania wengi kuujua ukweli.


Mkurugenzi wa shirika la Uraia na msaada wa kisheria(CILAO) Odero Charles aliomba tume hiyo, kutenda haki katika sakala hilo kwani kuna matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binaadamu ikiwepo wananchi kuporwa ardhi na mmoja kupotea.


"Tunaimani kubwa na tume hii kutoa taarifa ya haki ambayo itakwenda kuondoa tatizo la migogoro ya ardhi hasa pale ambapo serikali inakiuka sheria na kuchukuwa ardhi ya wananchi bila maridhiano kwa madai ya kufanya uhifadhi ama kuwapa wawekezaji"alisema.


Tume ya Haki za binaadamu na Utawala bora imefika Arusha na kutembelea Loliondo na Ngorongoro, ikiwa ni takriban miezi mitatu tangu tume ya afrika ya haki za binaadamu nayo kutembelea maeneo hayo kuzungumza na wananchi kuhusiana na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binaadamu.

 Mwisho

Post a Comment

0 Comments