SERIKALI YAUPIGA PINI MGODI WA TANZANITE WA MFANYABIASHARA MZITO ARUSHA NI BAADA YA KUIBUKA VURUGU ZILIZOPELEKEA MAOFISA WATANO WA SERIKALI KUCHEZEA KICHAPO KIKALI

 

Menard Msengi afisa madini Mkazi Manyara

Na Joseph Ngilisho,ARUSHA 


Afisa Madini Mkazi Mkoani Manyara (RMO),Mhandisi Menard Msengi amesema kuwa ofisi yake imechukua hatua ya kuufunga mgodi wa kitalu B wa madini ya Tanzanite unaomilikiwa na kampuni ya Gems and Rock Venture unaodaiwa kuingilia mgodi wa kitalu C ili kupisha uchunguzi na upimaji wa mpaka.

Alisema hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache mara baada ya kuibuka vurugu za kugombea mpaka baina ya kampuni hizo na kusababisha vurugu zilizopelekea maofisa watano wa serikali kipigwa na kuumizwa vibaya wakiwemo wachimbaji wadogo wakati wakizuia madini yasipelekwe kuthaminishwa.

Alisema siku ya tukio Machi 13 mwaka huu maofisa wa serikali walienda kufanya ukaguzi ili kujiridhisha eneo linagogombewa ni mali ya nani na walipofika eneo la tukio walikuta kampuni ya Gems and Rock Venture ikiendelea na uchimbaji na walikuwa wamepiga baruti na kupata madini ambapo maofisa hao waliagiza madini hayo yakathaminishwe katika ofisi za madini zilizopo Mererani. 

Hata hivyo wafanyakazi wa kampuni hiyo waligoma kuachia madini hayo walidai ni mali ya mgodi wao  na kuibua vurugu zilizopelekea baadhi ya watu kupigwa na baadaye polisi walifika eneo hilo na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wachimbaji hao akiwemo Saitoti .

Mhandisi Msengi alifafanua kuwa  tangia 
Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD ipate leseni ya uchimbaji katika mgodi huobmwaka jana ,hapakuwahi kutokea malalamiko yoyote ya mipaka ya uchimbaji.

"Tumelazimika kwenda kupima upya eneo hilo na kwa sasa hatua za awali tumeamua kusimamisha uchimbaji katika mgodi wa Gems and Rock Venture "alisema.

Aliwataka wachimbaji kuheshimu mipaka ya uchimbaji kwenye migodi yao ili kuepuka migogoro inayoweza inayoweza kuhatarisha amani.

"Tukijiridhisha madini hayo waliyapata kinyume na utaratibu yatataifishwa na  hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa kuwa awali tuliwahi kuiandikia barua kampuni ya Gems and Rock Venture kuhusiana na ukiukwaji wa uchimbaji kwenye mipaka"

Naye kamanda wa polisi Mkoani humo,George Katabazi  alisema jeshi la polisi  linamshikilia mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite , Joel Saitoti Mollel ambaye pia ni Meneja wa Kampuni ya Gem and Rock  kwa kuwajeruhi kwa kipigo watumishi watano wa Serikali na wafanyakazi wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD.

Pamoja na Saitoti polisi pia inawashikilia wachimbaji wengine 21 wa kampuni hiyo ya Gem and Rock Venture kwa kuwajeruhi watumishi hao wa serikali na wafanyakazi wa Franone.

Inadaiwa kuwa Saitoti na wenzake 21 wamewajeruhi watumishi hao wa serikali na wafanyakazi wa Kampuni ya Franone Mining chini mgodini wakitumia silaha za jadi na vitu vyenye ncha kali

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi akizungumza tukio hilo amekiri kushikiliwa na polisi kwa wachimbaji hao akiwemo mfanyabiashara Saitoti.

Kamanda Katabazi alifafanua kiwa Saitoti na wafanyakazi wenzake 21 wa kampuni hiyo wanadaiwa kufanya tukio hilo Machi 13 kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani, Kitalu C.

Alisema wachimbaji hao ambao mgodi wao upo kitalu B (Opec) walifanya tukio hilo kwenye mgodi wa kitalu C unaomilikiwa na mwekezaji Kampuni ya Franone Mining ambaye anaubia na serikali .

"Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kisha tutawafikisha mahakamani kujibu mashtaka hayo," alisema kamanda Katabazi.

Endsss

Post a Comment

0 Comments