JIJI LA ARUSHA FUNGA KAZI , LAMWAGA MABILIONI KWA VIKUNDI 169..MEYA :HII HAIJAWAHI KUTOKEA TUMEWEKA HISTORIA


Na Joseph Ngilisho, ARUSHA 

VIKUNDI 169 kati ya 205  vya wajasiriamali katika Halmashauri ya Jiji la Arusha,vimepokea  mkopo wa shilingi bilioni 2.656 kutoka Halmashauri ya Jiji  kwa ajili ya kuboresha mitaji yao.


Kaimu mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Hargeney Chitukuro ameyasema hayo kwenye hafla ya kukabidhi hundi hiyo iliyoshuhudiwa na mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisian Mtehengerwa .


Alisema kuwa jumla ya Vikundi,205 viliwasilisha maombi ya mkopo huo na uhakiki ulifanyika ambapo vikundi  127 vya wanawake vimepata mkopo wa shilingi bilioni 1,954 000,000,Vikundi 32 vya vijana mkopo thamani ya shilingi 602,000,000 ,
Vikundi 10 vya walemavu vimepata mkopo wa shilingi 100,000,000.


Aliongeza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya wakopaji kushindwa kujeresha mkopo  kwa wakati na kwamba  tangia wameanza kukopesha jumla ya mikopo yenye thamani ya sh,bilioni 14 imetolewa huku nusu ya fedha hizo zikishindwa kurejeshwa kutokana na sababu mbalimbali.


Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Felisian Mtehengerwa aliipongeza Halmashauri hiyo kwa kuboresha kiwango cha mkopo kwa ajili ya makundi hayo na kufikia kiasi cha sh,bilioni 2.6 kiwango ambacho hakikuwahi kutokea na kuitaka Halmashauri hiyo kutumia mfumo wa kidigitali kuwasajiri wakopeshwaji ili kuepuka udanganyifu wa marejesho.


Alitoa rai kwa vikundi vinavyochukua mikopo kuhakikisha mikopo hiyo inawakomboa vijana ,wanawake na walemavu kutoka kwenye hali duni hadi maisha bora na inarejeshwa kwa wakati.

"Wote waliopokea fedha za mkopo hakikisheni mnafanya biashara zenye tija na zenye ubunifu na msifanye biashara za mazoea ili mrejeshe fedha hizo kwa wakati ili watu wengine wakopeshwe"


Aidha aliitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha inafuatilia kiasi cha sh,bilioni 7 ambazo hazijarejeshwa kati ya sh,bilioni 14 zilizokopeshwa ili kuwapatia fursa watu wengine wenye uhitaji waweze kukopeshwa.

Awali meja wa jiji la Arusha,Maximilian Iranghe alisema hatua ya jiji la Arusha kutoa mkopo wa sh,bilioni 2.654 kwa makundi ya vijana ,wanawake na walemavu ni hatua nzuri iliyotokana makusanyo ya mapato ya ndani na wameweka historia ya aina yake ambayo haikuwahi kutokea.


Meya huyo aliwashukuru wafanyabiashara kwa kuendelea kulipa kodi ipasavyo na kuongeza kuwa jiji la Arusha lina nia njema ya kuendelea kutoa mikopo nia ni kuhakikisha watu wote wenye uhitaji wananufaika na kuboresha vipato vyao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arusha,Dkt Wilfred Solel alisema ni vema suala la mikopo likawa wazi ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi waliowengi kujiunga na vikundi na kunufaika na mikopo hiyo. 


"Suala la mikopo 
ni vizuri likawa wazi na ukweli hatua  itakayosaisia kuondoa manung'uniko ili kila mmoja apate fursa ya kuondoa makali ya maisha"

Naye mwenyekiti wa vccm wilaya ya Arusha ,Hasan Mndeme aliishukuru halmashauri ya jiji la Arusha kwa kutenga kiasi hicho cha fedha kupitia mapato yake ya ndani na kutoa mkopo kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana.



Aliwasihi vijana kuwa na mwamko wa kuunda vikundi ili kupata fursa ya kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri ya jiji la Arusha itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia biashara zao.


"Tumeona mabadiliko kwa vijana tangia wameanza kupokea mkopo, wengi wao vipato vimeongezeka  ,rai yangu kwa vijana wawe warejeshaji wazuri ili na wengine waweze kukopeshwa  "






 














Post a Comment

0 Comments