Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Kauli ya mbunge wa zamani jimbo la Arusha,Godbless Lema kuhusu sekta ya bodaboda kutokuwa na tija katika maisha , imezua sintofahamu kwa baadhi ya waendesha pikipiki ambapo wamejigamba kuwa wao ni matajiri kuliko hata mshahara wa polisi.
Machi 1,2023 akihutubia mkutano wa hadhara ,Lema alisema kazi ya boda boda ni kazi ya laana serikali inapaswa kutengeneza ajira za vijana zinazoeleweka na sio kufukuza upepo kama wanavyofanya bodaboda kwani baada ya miaka 60 wanaweza kupata athari za kiafya.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Kaloleni jijini hapa,Mwenyekiti wa bodaboda Okero Costantine alisema kuwa kazi ya boda boda ni kazi kama kazi zingine na sio kazi ya laana kama alivyosema Lema na inapaswa iheshimiwe .
"Kuna kauli tata zilizotolewa na mh.Lema kuweza kukashfu umoja wetu na kauli hizo sisi kama viongozi hazikuweza kutufurahisha ikiwemo kuwa bodaboda sio ajira kazi ya kufukuza upepo ni umaskini mtupu"
Aliongeza kwa kudai kwamba bodaboda ni kazi kama kazi nyingine na inafanyika katika nchi nyingi za Afrika Mashariki,hivyo tunamwomba Lema aombe radhi na aelekeze ajira mbadala.
Naye katibu wa Uboja,Hakimu Msemo,alisema vijana wengi wameacha kazi zao za zamani(Wizi) na kuqmua kujiajiri kwenye ajira ya bodaboda baada ya kukosa ajira rasmi.
Msemo alimtaka Lema kuja na hoja mbadala zitakazoweza kuwasaidia vijana kujipatia kipato na sio kwa masimango.
Kuhusu Uboja kutumika kisiasa ,Msemo alisema kuwa wao ni sekta huru na hawapo kwa ajiri ya kutumiwa na wanasiasa .
Alisema milango ipo wazi kwa wanasiasa wanaotaka kuwasaidia kupatikana kwa fedha zao sh,milioni 400 zilizoibiwa kwenye akaunti yao na watu wasiojulikana.
Katibu huyo alisema kuwa bodaboda sio kazi ya kuidharau kwani wengi wao ni matajiri wanamiliki nyumba,magari kuliko hata mshahara wa polisi.
Katika hatua nyingine Uboja wamedai kuwa sakata la wizi wa fedha zao sh,milioni 400 wamedai kuwa suala hilo lipo kwenye hatua nzuri na linashughulikiwa na vyombo vya dola na wamemkaribisha lema kuwasaidia ili kupata haki yao.
Ends....
0 Comments