Na Joseph Ngilisho BABATI
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander pamoja na aliyekuwa Ofisa mtendaji wa kata ya Emboreet wilayani Simanjiro, Belinda Sumari wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na Kampuni ya Uwindaji ya HSK Safaris Ltd.
Babati. Mbunge wa Misungwi Mkoani Mwanza, Alexander Mnyeti amesomewa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Hata hivyo, Mnyeti hakuwepo mahakamani wakati kesi yake iliposomwa mjini Babati ,jana Februari 7, 2023 dhidi ya Kampuni ya Uwindaji ya HSK Safaris Ltd ya Wilaya ya Simajiro, kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara kampuni hiyo.
Wakili wake Kuwengwa Ndojekwa ambaye aliiomba mahakama mbele ya Jaji Mfawidhi, John Kahyoza imruhusu aiunganishe serikali kwenye kesi kwa sababu yale anayotuhumiwa kuyatenda yalitendeka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na alikuwa mtumishi wa umma.
Mnyeti anadaiwa kushirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Emboreet, Belinda Sumari na Salehe Alamry kuinyang'anya kitalu cha uwindaji Kampuni ya HSK Safaris Ltd bila kufuata sheria.
Katika shauri hilo namba 2 la mwaka 2022 wadaiwa katika shauri hilo ni Alexander Mnyeti mdaiwa namba moja, mdaiwa namba mbili Belinda Sumari aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Emboreet wilayani Simanjiro na mdaiwa wa tatu Salehe Alamry.
Katika shauri hilo namba 2/2022 la madai Mnyeti anawakilishwa na wakili Kuwengwa Ndejekwa, Salehe Alamry anawakilishwa na wakili Sheki Mfinanga na HSK Safaris Ltd anawakilishwa na Edmond Ngemela.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Wakili wa Alamry alitakiwa kuchukua nyaraka na hatua stahiki za kuitwa shaurini ila badala yake alikuja na maneno matupu.
Vilevile mahakama ilibaini Salehe Alamry alipokea hati ya kuitwa shaurini ila kwa kiburi alikataa kuzipokea.
Jaji Kahyoza amesema pamoja na kuwaruhusu wajibu madai ndani ya siku 10, ameona kuna sababu za ucheleweshaji zisizo na msingi hivyo ameamuru wakili wa Alamry kulipa Sh300,000 ambapo Sh150,000 alipwe wakili wa Kampuni ya HSK Safaris Ltd, Sh100,000 alipwe wakili wa Mnyeti na Sh50,000 alipwe Belinda Sumari kwa usumbufu.
Jaji aliahirisha shauri hilo hadi Machi 3 mwaka huu ili kuendelea kusikilizwa tena
0 Comments