SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA LAWAFIDIA WAKULIMA NA WAFUGAJI MILIONI 557 ,WALIOPOTEZA MAZAO NA MIFUGO KWA UKAME

 


Na Joseph Ngilisho,ARUSHA 

Shirika la Bima la Taifa (NIC),limelipa fidia kiasi cha sh,milioni 257.3 kwa wakulima wa Nafaka AMCO'S, wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baada ya kupata hasara katika kilimo cha ngano katika msimu uliopita, kutokana na ukame uliyoyakumba maeneo mengi wilayani  humo.

Mbali na wakulima hao wa Nafaka Amcos ,shirika hilo pia limelipa  fidia ya sh, milioni 300 kwa wakulima 6000 na wafugaji 1000 waliojiunga na bima baada ya kupata hasara ya ukame. 


Akiongea katika hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya sh,milioni 257,385,779.50 kwa wadau wa  kilimo wa nafaka Amco's mwishoni mwa wiki ,Mkurugenzi Mtendaji wa NIC,Dkt Elirehema Doriye alisema hatua ya kulipa fidia kwa wanachama wake  wanapopata hasara ni utaratibu wa kawaida wa Shirika hilo.

"Siku hii ya leo tumekutana hapa ili kuwakabidhi AMCO's  sh,milioni 257 kama fidia ya uwekezaji wa sh,milioni 500 walioufanya kwenye kilimo cha nafaka baada ya mazao yao kukumbwa na ukame mkali wa jua"


Alisema kuwa shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa wakulima na wafugaji ili wajiunge na bima ili kuweza kunufaika na fidia pindi kunapotokea changamoto za majanga mbalimbali ikiwemo ukame na hivyo kunusuru mitaji yao.

"Tumetoa elimu ya bima ya kilimo kwa wakulima 10,000 na  kati yao, wakulima 6000 walikata bima ya kilimo na wafugaji 1000 walijiunga na bima'' ,

Hata hivyo alisema wakulima hao na wafugaji walipata hasara baada ya mazao yao kuungua na jua na mifugo kufa kwa ukame,ambapo shirika hilo liliwafidia kiasi cha sh, milioni 300 iliyowasaidia kupunguaza ukali wa maisha.

Alisema mwitikio wa wakulima na wafugaji ni mkubwa katika kujiunga na bima japo bado baadhi yao hawaamini hadi pale wanapoona wenzao tunalipwa fidia .

Hivyo kupitia vyama vya ushirika na mifumo yao ya uongozi wanaweza kupata elimu ya bima ili wajiunge na bima na kujiweka salama katika shughuli zao za kilimo na ufugaji.

Naye meneja wa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko  kanda ya kaskazini, Peter Mobe aliwataka wakulima wanaochukua mbegu za mkopo katika bodi hiyo kujiunga na Bima ili kuepuka hasara zisizo na tija.

Meneja wa NMB tawi la Siha, Frank Kilas qmbao ndiyo walitoa mkopo huo amesema kuwa walipoanza mchakato wa kukatia bima wakulime wengine walikuwa wagumu kuelewa isipokuwa Nafaka AMCOS wenyewe walibali kukata bima ya mazao hivyo wakawakopesha fedha za kulimia zao la ngano.

"Kwa tukio la wakulima hao kufidiwa na NIC inapeleka ujumbe mzito kwa wakulima wengine kuelewa kuwa wanapokata bima ya mazao wanaweza kufidiwa endapo yatatokea majanga ya asili yatakayowasababishia hasara kwenye kilimo,"

Kilas alisema kuwa NMB inafanya kazi na makampuni 10 ya bima ikiwemo NIC katika kukatia bima mbalimbali ikiwemo bima za kilimo, magari,  nyumba na nyinginezo.



Ends...






Post a Comment

0 Comments