Na Joseph Ngilisho Arusha
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imemhukumu kifungo cha miaka minne jela aliyekuwa mtumishi wa shirika la umeme Tanesco, Ombeni Alphayo (35) na kumlipa fidia Sh milioni 15 , baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kujaribu kumuua aliyekuwa mke wake, Veronica Kidemi ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sokoni II.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Joachim Tiganga, wakati shauri hilo la jinai namba 30/2021 lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji ,hata hivyo mshtakiwa alikiri kosa na hivyo kuirahisishia kazi mahakama na hivyo kutoa adhabu hiyo.
Mahakamani hapo Jamhuri ilikuwa inawakilishwa na Mawakili wa Serikali Grace Madikenya na Charles Kagirwa huku mshitakiwa huyo akiwakilishwa na Wakili Richard Manyota.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Tiganga alisema chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu mshitakiwa akikutwa na hatia ya kosa baada ya kukiri kosa mwenyewe, inasema anatakiwa kupewa adhabu ya juu kifungo cha maisha huku akinukuu mashauri kadhaa ya Mahakama ya Rufaa.
Alisema mtuhumiwa huyo aliyekuwa anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 25, 2020 nyumbani kwake, kinyume na kifungu cha 211 cha sheria ya kanuni ya adhabu, ambapo baada ya kuangalia hoja za pande zote imemtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela na kutakiwa kulipa fidia ya Sh15 milioni.
Alisema katika kutoa hukumu mahakama inatakiwa isiangalie ukubwa wa kosa pekee bali itazame shufaa zilizotolewa na mshtakiwa pamoja na kutumia busara na kuangalia iwapo ni mkosaji wa mara ya kwanza.
"Mahakama inaona mshtakiwa anatakiwa kuonewa huruma japo wakili wake aliomba apewe adhabu mbadala ila mahakama inaona adhabu mbadala haitatenda haki," alisema.
"Mahakama inaona kwamba adhabu ya jela ndiyo adhabu mwafaka, hasa ikizingatia mshtakiwa anayo majukumu ambayo mahakama ya chini imempata ya kutunza familia hasa watoto.
"Mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka minne jela na baada ya hapo kwa kuzingatia ukweli mhanga amepoteza kiungo inatoa amri ya fidia Sh15 milioni kwa mwathirika, nafahamu fedha huenda isitibu wala isitoshe na kiungo cha binadamu hamna fedha inarejesha hiyo ni kifuta jasho, na kama kuna ambaye hajaridhika na uamuzi anaweza kukata rufaa," alisema.
Aidha shauri hilo lilipangwa leo na kesho kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ambapo upande wa Jamhuri ulikuwa umepanga kuwa na mashahidi watatu, ambapo baada ya shauri kutajwa upande wa utetezi uliomba kukumbushwa shtaka linalomkabili mtuhumiwa huyo ambaye baada ya kusomewa alikiri kutenda kosa hilo la kujaribu kumuua mke wake kwa kumkata kiganja cha mkono wa kulia, kujeruhi mkono mwingine ambao umewekewa chuma kwa sasa.
Ends .....
0 Comments