Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dkt Pindi Chana amesisitiza kuwa lengo la serikali la kufikisha watalii milioni tano, mwaka 2025 lipo pale pale baada ya sekta ya utalii nchini kuendelea kuimarika na kufikisha watalii milioni 1.2 mwaka 2022 ukilingamisha na watalii 922,682 mwaka 2021.
Ongezeko hili la watalii ni sawa na asilimia 71.02 kuanzia Januari hadi Novemba 2022, ambapo Serikali imeweka lengo kuwa ifikapo mwaka 2025 ipokee watalii milioni tano kwa mwaka na mapato kufikia Dola bilioni 6.
Waziri Chana aliyabainisha hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) uliolenga mashauriano baina ya sekta binafsi na sekta za umma katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Dkt Chana alisema ongezeko hilo la watalii limetokana na jitihada za Serikali na wadau wa utalii, zikiwemo kukuza, kuendeleza na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kwa kutumia Programu ya ‘The Royal Tour.’
Alisema ongezeko hilo limechangiwa na uboreshaji wa miundombinu ya utalii, hudumaa na kuimarisha matumizi ya Tehama.
Akizungumzia mkutano wa mwisho wa baraza hilo, uliofanyika Julai, 2022 alisema yaliwasilishwa maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano wa 13 wa TNBC Maeneo, ambapo yaliyoainishwa ni pamoja na mapitio ya Sheria ya Utalii Namba 29 ya mwaka 2008, uboreshaji wa mifumo ya malipo ili kuwezesha kuwa na dirisha moja la malipo.
Akitoa mrejesho wa jitihada za Serikali kutatua changamoto katika sekta ya Utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara nyingine zimetatua baadhi ya kero na nyingine zipo katika mchakato.
Alisema kulikuwa na hoja 24 zilizotolewa katika mkutano uliopita na nyingi zimepatiwa ufumbuzi, ikiwepo kupunguza idadi ya kaguzi, kuwepo kwa dirisha moja la malipo na ada katika sekta hiyo, lakini pia kuongeza muda wa dhamana kutoka siku 30 hadi 90.
Akizungumzia changamoto ya malipo ya wapagazi na mishahara katika sekta ya utalii, alisema tayari wizara ilifanya mazungumzo na Wizara ya Kazi, ambapo idara ya kazi imepewa jukumu la kufanyia kazi changamoto ya mikataba ya wapagazi na malipo yao.
Kuhusiana na malipo ya waongoza watalii kupunguzwa kutoka dola 50 hadi 20 kwa mwaka, alisema jambo hilo ni la kisheria, lakini linaendelea kufanyiwa kazi, huku pia suala la malazi katika hifadhi na kambi za kitalii linaendelea kupata ufumbuzi.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa chama cha wapagazi (TOP), Loshiye Mollel aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii, kupatia ufumbuzi malipo na stahiki za wapagazi zaidi ya 20,000 wanaofanya kazi kusaidia watalii mlima Kilimanjaro.
Ends...
0 Comments