Na Joseph Ngilisho, ARUMERU
WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameipa wiki mbili Kampuni ya Madini ujenzi ya Rocktronic Ltd inayochimba kokoto wilayani Arumeru,mkoani Arusha, kuandaa mpango wa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo kuiwezesha jamii kunufaika na rasilimali hiyo ikiwemo utunzaji wa mazingira.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki wakati alipotembelea machimbo hayo yaliyopo eneo la King'ori katika halmashauri ya Meru ,wilayani humo na kueleza kufurahishwa na mradi huo.
Dkt. Biteko alisema, mpango huo utasaidia kuwa na malengo ya huduma kwa jamii ili kuleta maendeleo na kuondoa migongano inayoweza kujitokeza siku za baadaye na wakazi wa eneo hilo. Aliongeza kuwa mpango huo utasaidia katika kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Aidha, alitaka kampuni hiyo kuandaa taarifa ya upembuzi yakinifu ili kuiwezesha kujua muda wa uhai wa mgodi, kiasi cha mapato kitakacholipwa kwa Serikali.
Akizungumzia utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko ameielekeza kampuni hiyo kuanza kupanda miti katika maeneno ya machimbo ili kuhifadhi mazingira. Alitoa wiki mbili za kuanza kupanda miti na kuitaka kampuni hiyo kuajiri afisa mazingira.
Alisisitiza kampuni hiyo, kuandaa mpango wa uchimbaji ili kuacha kuchimba kwa kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine na kueleza kuwa mpango huo utasaidia kuwa na uchimbaji wenye tija na endelevu.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Rocktronic Ltd Prajesh Chauhan alisema kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutoa ajira ndani ya kata ya Malula kwa wazawa wenye ujuzi na wasio na ujuzi wapatao 118.
Katika hatua nyingine alisema kampuni imechangia shughuli za maendeleo ndani na nje ya kata kwa kutoa vifaa mbalimbali kama vile kokoto, mawe, vifusi na fedha ili kusaidia miradi ya maendeleo ya wananchi katika Sekta ya elimu, afya, maji na barabara za ndani ya vijiji.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha Mhandisi Alphonce Bikulamchi alisema Ofisi ya Madini Arusha itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya Arumeru na Mkurugenzi kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za uchimbaji madini.
Ameongeza kwamba, ofisi itaendelea kutoa elimu juu ya Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake pamoja na miongozo mingine ya Serikali ili kuchangia ukuaji wa Sekta ya Madini kwa ujumla.
Ends....
0 Comments