WAKULIMA WA VITUNGUU WACHAFUA HEWA MANG'OLA,WANANCHI WACHARUKA


Na Joseph Ngilisho ,KARATU 


WANANCHI katika kata tatu wilayani Karatu mkoani Arusha,wamedai afya zao zipo hatarini kufuatia uwepo  wa mashamba makubwa ya Vitunguu yanayolimwa katika makazi yao, ambapo wamiliki wake hutumia viatilifu vya sumu kuua wadudu waharibifu na hivyo kuathiri afya zao na baadhi yao kupata madhara ya kupumua.


Aidha athari hiyo pia imekuwa ikiwakumba wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Qand'end, wagonjwa wanaotibiwa katika zahanati ya Lake Eyasi na nyumba za kulala wageni zilizozungukwa na mashamba hayo.


Wakiongea kwa nyakati tofauti mara baada ya waandishi wa habari kutembelea katika kata hizo za Mang'ola kujionea athari hizo , baadhi ya wakazi hao, kutoka kata za Endamag'a Mang'ola na Baray ,Paselina John na Mathayo Babo walidai kuishi maisha ya tabu kutokana na dawa zinazopuliziwa kuua wadudu kwenye vutunguu.


"Kwakweli sisi wakazi wa Baray tunapata tabu sana siku hizi kila eneo limegeuzwa shamba la tutunguu hadi kwenye makazi ya watu,wakianza kupuliza dawa za sumu ,watoto wetu wanakohoa na kubanwa vifua hata shule hawaendi"alisema Paselina 


Aidha ameiomba serikali kuwanusuri kwa kuwa malalamiko yao wameyafikisha ngazi mbalimbali lakini hawajapata ufumbuzi huku wakiendelea  kudhulika. 


Matayo Babo mkazi wa Kitongoji cha Mbuyuni aliwatuhumu viongozi wa vijiji kuruhusu uwepo wa mashamba hayo kwenye makazi ya watu wakati wanafahamu kuwa hupuliziwa viatilifu vya sumu kwa ajili ya kuua wadudu.


"Hapo awali mashamba ya vitunguu yalijitenga umbali na makazi ya watu lakini watu wamevamia maeneo na kufanya uharibifu wa mazingira kwa kufyeka miti ya asili na kulima ovyo mashamba ya vitunguu"alisema.


Aidha ameiomba serikali na mamlaka zake kufika kijijini hapo ili kujionea athari hizo kwani wamiliki wa mashamba hayo sio wakazi badala yake wamekuwa wakiyakodisha  kwa wazawa na kubadilisha matumizi kwa kulima zao la vitunguu.


Katika hatua nyingine wakazi hao wamelalamikia uwepo wa raia wa nchi jirani ya Kenya ambao wamekuwa wakikodisha maeneo kutoka kwa wanakijiji na kulima kilimo cha vitunguu jambo ambalo limeongeza utitiri wa mashamba hadi kwenye  makazi hayo.


"Hivi sasa wakenya wamejaa sana hapa Mang'ola na wanakodisha mashamba na kulima vitunguu ndio maana miti inafyekwa kila kukicha na kutengenezwa vitalu vya  vitunguu hali ambayo inasabaisha hali ngumu kwa sisi wakazi pindi wanapokuwa wakipuliza dawa za kuua wadudu"alisema Thomas Gwandu mkazi wa Mang'ola Barazani


Mwananchi mwingine Magreti Male alisema amekuwa akiishi kwa shida yeye na watoto wake kupata mafua ya mara kwa mara na kubanwa vifua jambo ambalo alidai ni kutokana na athari ya dawa hizo zinazopuliziwa katika mashamba hayo na kuiomba serikali kuwanusuru na adha hiyo.


"Mimi nina watoto wanne na wote ni wadogo hawaishiwi na mafua ya mara kwa mara na nikienda hospitalini naambiwa wanatatizo pia la kupumua na hii ni kutokana na madawa hayo yanayopulizwa kwenye  mashamba ya vitunguu"


Naye muuguzi mkuu katika Zahanati ya Lake Eyasi dkt Magreth Madila alisema kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wanaokuja kutibiwa katika zahanati hiyo huwa wanakutwa na tatizo la mfumo wa upumuaji na hii ni kutokana na athari za viatilifu vya dawa za kuua wadudu kwenye mashamba ya vitunguu.


"Magonjwa mengi ya kujirudia katika zahanati yetu ni tatizo la mfumo wa kupumua kunakosababishwa na dawa za sumu zinapopilizwa katika mashamba ya vitunguu yanayotuzunguka"


Aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya Kilimo cha kitunguu ili kutofautisha makazi na mashamba na kuepusha kuepusha athari zinazotokana na viatilifu vya sumu.


Mmoja ya walimu katika shule ya msingi Qand'end, ambaye  (jina Lake limehifadhiwa)alidai kuwa shule yao imezingukwa ma mashamba ya vitunguu, hivyo kuwaathiri wanafunzi na walimu wawapo shuleni hapo.


Alisema meneo mengi yenye uoto wa miti ya asili yamekuwa yakifyekwa na kutengenezwa mashamba ya vitunguu na miongoni mwa maeneo hayo ni ni pamoja na yale yaliyopo kando na shule hiyo na kuifanya shule hiyo kuwa katikati yaa mashamba ya vitunguu.


Diwani wa kata ya Baray, Elitumaini Rweyemamu alisema kuwa malalamiko hayo yalishafikishwa ofisini kwake na aliyapeleka kunakohusika ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira  NEMC.


"Nimepata malalamiko ya wananchi juu ya athari ya madawa ya kuuwa wadudu yanayopuliziwa kwenye mashamba ya vitunguu hatua za awali ni kuandaa mkutano mkuu wa wananchi "alisema.


Hata hivyo alisema yeye hana mamlaka ya kuzuia mtu kulima zao lolote kwenye shamba Lake ispokuwa amepanga kuandaa mkutano mkuu wa wananchi ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo.


Mkuu wa wilaya ya Karatu ,Dady Kolimba alipoulizwa alisema hana taarifa hiyo ila alimwomba mwandishi wa habari kuambatana naye kwenye mashamba hayo kujua kero za wananchi. 


"Mimi sina taarifa hiyo ila ni vizuri wewe mwandishi ukanichukua ili twende sote tukajionee kero hiyo"alisema.


Ends..



.














Post a Comment

0 Comments