Na Joseph Ngilisho, KARATU
JAMII ya Wahadzabe na Wadatoga wanaoishi wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha,wametishia kuyahama makazi yao mara baada ya halmashauri ya wilaya hiyo, kutangaza tozo mpya ya mapato ya utalii ,iliyopunguza maslahi yao .
Aidha wamesema hawatatoa ushirikiano kwa mtalii yoyote atakayeingia kutembelea jamii yao na wamemtaka waziri wa Mali asili na Utalii,dkt Pindi Chana kufika haraka wilayani humo ili kutatua mgogoro huo na halmashauri .
Wakiongea na waandishi wa habari katika kijiji cha Qand'end kata ya Baray ,Ntontowasi Nuika na Kankono Thomas kutoka jamii ya wahadzabe, walisema kuwa halmashauri yao imepitisha sheria mpya ya tozo za watalii inayokandamiza bila kuzingatia maslahi yao na hivyo hawapo tayari kuona wakitumika wakati wanamajukumu mengi ikiwemo kuendeleza tamaduni zao.
Walisema halmashauri hiyo imepitisha kila mtalii anayeingia katika lango la kijiji cha Qand'end kufanya shughuli za utalii, ikiwemo kuiona jamii ya wahadzabe ,wadatoga na wahunzi,kulipa dola 25 na kiasi hicho kikigawanywa, jamii hiyo inaambulia dola 2 ,tofauti na hapo awali ambapo kila gari la utalii lililipa dola 110 na jamii hizo zikipata dola 20 kila moja.
"Ujio wa mkuu wa wilaya kwenye kikao cha jana ulikuwa wa mabavu kutukandamiza sisi ili tukubaliane na ile bei ya tozo ambayo wao walioipitisha bila kutushirikisha,sisi kama Wahadzabe tumeogopa kwani hatujawahi kuona bunduki"alisema Ntontowasi.
Alisisitiza kuwa jamii yao kwa sasa inajitambua na hawapo tiyari kuona ikitumika ama mshumaa kwa maslahi ya wachache wakati wao ndio chanzo cha watalii kuingia kijijini hapo. Ameiomba serikali kupitia waziri mwenye dhamana kukutana na jamii hiyo haraka kabla hawajatekeleza maamuzi yao.
"Msimamo wetu iwapo serikali itashindwa kutusikiliza hatutatoa ushirikiano kwa watalii na tutahama maeneo haya ,tumechoka kutumika kama kalai la zege wakati sisi ndio kivutio cha watalii "alisema .
Jamii hiyo ilimtupia lawama mkuu wa wilaya ya Karatu,Dady Kolimba kwa kushindwa kuwasikiliza wawakilishi wao alipokutana nao ikiwemo diwani wao,Elitumaini Rweimamu badala yake alitumia mabavu kushinikiza tozo hizo zianze kutumika mara moja huku akiwatisha kuwasweka ndani watakao kwenda kinyume na maenekezo yake.
"Juzi usiku mkuu wa wilaya alikuja hapa kwetu akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama na askari wengi wenye silaha za moto, viongozi wetu walikwenda kumsikiliza lakini hakuna aliyepewa nafasi ya kutoa maoni yake,badala yake watu wetu walitishwa kwa kuambiwa watawekwa ndani na wengine wawili walikamatwa na kwenda kuwekwa ndani "alisema Kankono.
Naye Sabargwa Dandu kutoka jamii ya Wadatoka,alisema kuwa hawakubaliani na tozo mpya ya dola 25 kwa utalii wa Lake Eyasi akidai hawajashirikishwa na mabadiliko hayo na wao kama wadau wa utalii wameona hayana tija kwao.
Alimwomba waziri wa Mali asili na Utalii kuitembelea jamii hiyo ambayo haikubaliani na gawio la dola mbili kati ya dola 25 alizotozwa mtalii wakidai kwamba huo ni uonevu unaolenga kudhorotesha mila na desturi za makabila hayo adimu hapa nchini.
Diwani wa kata ya Baray,Elitumaini Rweimamu alisema kuwa hakuna kikao hata kimoja cha baraza la madiwani wilayani humo kilichoketi na kupitisha agenda ya mabadiliko ya tozo za utalii katika lango la Qand'end.
"Ni kweli hizo tozo zimeleta changamoto kwa jamii kwa sababu hapakuwa na ushirikishwaji wa mabadiliko hayo,na mimi kama diwani hakuna kikao hata kimoja tulichokaa na kukubaliana kila mtalii kutozwa dola 25 huo ni uongo labda kama ni baraza la madiwani la zamani"
Mkuu wa wilaya ya Karatu,Daddy Kolimba alisema kuwa makubaliano hayo yalipitishwa na baraza la madiwani na yeye kama mwakilishi wa serikali analazimika kusimamia na kuhakikisha amani inakuwepo na hawezi kutengua maamuzi ya baraza la madiwani.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Karatu, Karia Magaro alipohojiwa juu ya madai hayo alijibu kwamba tozo hiyo ilipitishwa mara baada ya makubaliano ya pande zote na waongoza utalii kupitia chama chao cha waongoza u TATO walishiriki kikao hicho.
"Kinachofanyika ni kwa ajili ya kuisaidia jamii ila changamoto iliyopo ni baadhi ya waongoza watalii kuwachochea wananchi walete vurugugu kwa maslahi yao"alisema.
Naye mwenyekiti wa kikundi cha waongoza utalii, bonde la ziwa Eyasi(LECTP),Joseph Awe alisema hawakubaliani na tozo hiyo mpya kwa kuwa haikulenga maslahi kwa wanufaika wa pande zote kwa sababu hakukuwa na makubaliano yoyote na kuishauri serikali kupitia upya maamuzi hayo kwa mustakabari wa kukuza sekta ya utalii nchini.
Alisema halmashauri hiyo ilipitisha tozo ya dola 25 kwa kila mtalii kwa mchanganuo kwamba waongoza watalii watapata dola moja,Wahadzabe dola 2,Wadatoga dola 2,wahunzi dola 2,Utawala dola 2,Vijiji saba kila kimoja dola moja ,na dola 10 kwa halmashauri jambo alilosema ni unyonyaji mtupu.
Ends....
0 Comments