Na Joseph Ngilisho, MONDULI
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Engaruka wilaya ya Monduli,mkoani Arusha,wamejeruhiwa vibaya kwa kipigo na baadhi yao kulazwa hopitalini mara baada ya kundi la wananchi wa kijiji cha Engaruka juu kuwavamia na kuwashambulia kwa mikuki na mawe wakiwatuhumu kutaka kupora maeneo yao.
Tukio hilo la aina yake ,limetokea juzi majira ya jioni wakati viongozi hao ,wajumbe wa kamati ya Siasa ya CCM kata hiyo walipoenda katika kijiji hicho kufuatilia mgogoro wa Ardhi na kukuta kundi la vijana,morani wa kimasai zaidi ya 30 waliokuwa wamejikusanya na kujihami kwa silaha za jadi , ambao baada ya kuwaona walianza kuwashambulia kwa mikuki na mawe.
Miongoni mwa viongozi waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa ccm kata hiyo,Leliya Sengeita pamoja na katibu wake Joseph Namoyo ambao walishambuliwa sehemu mbalimbali za miili yao na baadhi yao walipata majeraha ya kutobolewa jicho, kuvunjwa miguu,mikono na majeraha ya kichwa ,mbavu na uso.
Akizungumzia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Monduli ,Frank Mwaisumbe ,alidai kwamba jeshi la polisi wilayani humo limeanza uchunguzi na tayari wanamshikilia mwenyekiti wa kijiji hicho Abrahamu Logolie kwa upelelezi zaidi baada ya kuwepo taarifa kuwa ndiye aliyehamasisha wananchi wajikusanye.
Mwaisumbe ambaye pia ndio mwenyekiti wa ulinzi na usalama wilayani humo,alisema kuwa watu 7 walijeruhiwa vibaya na kupatiwa PF.3 na kwenda kutibiwa katika Kituo cha Afya kilichopo hapo Mto wa Mbu huku baadhi yao wakihamishiwa katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru jijini Arusha kwa matibabu zaidi.
Uchunguzi wa awali unabainisha kuwa chanzo cha vurugu hizo ni uchochezi unaofanywa na Mwenyekiti wa kijiji hicho ,Abrahamu Logolie (40), ambaye kamati ya siasa inamtuhumu kuuza baadhi ya maeneo ya kijiji hicho kiholela.
Kamati ilipopanga kwenda kufanya ukaguzi wa maeneo hayo, Mwenyekiti wa kijiji cha Engaruka juu anadaiwa kutuma vijana wa kimasai kuwazuia ili wasifanikiwe kukagua maeneo ya ardhi ya kijiji akiwaaminisha kuwa lengo la Kamati hiyo ni kutaka kuwapora ardhi yao.
Mkuu huyo alisema kuwa upelelezi wa sakata hilo bado unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika kutekeleza shambulizi hilo na ametuma timu ya askari polisi kutoka Monduli ikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi kwenda eneo la tukio kuongeza nguvu katika uchunguzi na ameagiza kuwakamata wote waliohusika na vurugu hizo.
Naye diwani wa kata ya Engaruka, Onesmo Naikoyo alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi baada ya viongozi wa chama kutembelea eneo hilo ili kujionea madai ya kuuzwa kwa baadhi ya maeneo.
"Viongozi wa ccm wa kata walipofika kule walikuta tayari wananchi wamejikusanya na kuanza kuwashambulia kwa mawe na mikuki kwa sababu hawakutaka wafike katika maeneo yao"alisema.
Alisema kuwa mgogoro huo umekuwepo kwa muda mrefu wa miaka miwili kwa sababu baadhi ya maeneo katika kijiji hicho yalivamiwa na kuuzwa kwa wananchi ambao sio wakazi wa eneo hilo.
Alibainisha kuwa kati ya majeruhi saba,watatu walihamishiwa katika hospitali ya mkoa Mt Meru ambapo baadhi yao walitobolewa macho ,kuvunjwa mkono na miguu.
Ends...
0 Comments