CCM YAMPA TANO SAMIA KURUHUSU MIKUTANO YA SIASA,BALOZI ASEMA WANACCM NDIO TATIZO


Na Joseph Ngilisho  Arusha.


JUMUIYA ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa,  imempongeza rais   Dk,Samia Suluhu Hasan  kwa  kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini kikidai itachochea maendeleo kwa taifa.

Aidha imesititiza kuwa ziara za nje wanazofanya Rais Dk, Samia  zinaleta tija zaidi kwani akirudi nchini harudi bure na zinafungua milango nje na ndani ya nchi.


Akiongea na vyombo vya habari jijini Arusha,mwenyekiti wa jumuiya hiyo Taifa ,Fadhili Maganya alisema fursa ya mikutano ya hadhara iliyotolewa na Rais Samia imeonesha ukomavu na uhuru wa demokrasia na  namna bora ya kuendesha siasa zenye tija hapa nchini.

Alisema, Rais alisema mikutano ya vyama vya siasa itumike kukosoa bila kugombana ikiwemo kuanza kukwamua mchakato wa katiba.

Alisema pia Rais ameridhia kuendelea kuangalia sheria mbalimbali kwaajili ya kuziboresha kwa maslahi mapana ya nchi na kuahidi ushirikishwaji wa wadau na makundi mbalimbali katika kuziboresha sheria hizo

"Tunatoa wito kwa watanzania wote kumtia moyo Rais Samia kwani umoja na mshikamano ndio msingi wa maendeleo katika nchi yetu"

Alitoa rai kwa vyama vya siasa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli za siasa hapa nchini ikiwemo kumuunga mkono kwakuendeleza siasa za maridhiano kwa maslahi mapana kwa mustakabali wa nchi.

Akizungumzia kuhusu safari anazozifanya Rais Samia nje ya nchi,Maganya alitumia methali ambazo ni mgaa,gaa na upwa hali wali mkavu na kusema kuwa mwenda bure si mkaa bure ,hivyo Rais anaposafiri kunafursa mbalimbali anafungua.

Kuhusu mikopo wanayodai anakopa kopa sana,Maganya alisisitiza kuwa Rais anakopa kwa maslahi ya Taifa na nchi kwa ujumla na mikopo inafanya kazi na kazi zinaonekana.

Naye mwenyekiti wa ccm Mkoa wa Arusha,Steven Zelothe alisema kuwa kuondoa katazo la mikutano ya hadhara ya kisiasa kumeleta faraja ,uzalendo ,ujasiri na uongozi imara nankuweka taifa imara.


Alisema kuwa ccm mkoa wa Arusha,inaunga mkono kwa dhati kuruhusiwa kwa mikutano ya siasa na kutaka mikutano hiyo isiende kuleta mtafaruku na kuvuruka amani ya nchi ambayo tumezoea kuwa nayo.

Hata hivyo alisema chama cha mapinduzi hakina hofu na mikutano ya wapinzani ila aliwataka wafanye siasa za kiungwana na ustaarabu  ili kuleta tija katika maendeleo ya wananchi. 


Naye kada wa ccm,balozi Daniel Njolaay alisema rais ameona mbali kuamua kuruhusu mikutano ya kisiasa akidai italeta changamoto kwa serikali na ushindani wa kisiasa.

Aliwataka wanachama wa ccm kuwa kitu kimoja kwa sababu baadhi yao ni tatizo lazima wajisafishe.

"Na sisi ndani ya ccm lazima tuwe kitu kimoja kwani matatizo yapo ndani yetu lazima tujitizame na tujisafishe"

Ends....






Post a Comment

0 Comments