MBOWE ATOBOA SIRI NZITO YA SABAYA,ASEMA MWAKA 2023 IWE MVUA IWE JUA


BY NGILISHO TV 

Hatutapoa 2023, hivi ndivyo unaweza kuelezea msimamo wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe kutangaza mambo matano ambayo kitayadai mwaka 2023.


Akizungumza na wanahabari baada idaba ya shukrani ya kuhamia katika nyumba yake mpya jana Alhamisi Desemba 29, 2022, Mbowe alisema mwaka 2023 watatumia mbinu zote zinazowezekana chini ya jua kudai Haki, Demokrasia, Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Ni katika nyumba hiyo ya ghorofa moja, ndipo ambapo Oktoba 19, 2020 asubuhi, genge la watu wenye silaha lilivamia nyumba hiyo wakijifanya ni askari wanaotaka kufanya upekuzi ambapo risasi za moto zilifyatuliwa na mtu mmoja kujeruhiwa.

Genge hilo lilihusishwa na mkuu wa wilaya wa wakati huo, Lengai Ole Sabaya lakini alipoulizwa alikanusha uwepo wa tukio hilo na kusema kilichotokea ni genge la Mbowe kulazimisha kupandisha bendera za Chadema kwenye makazi ya watu.

Ni genge kama hilo lilidaiwa usiku wa manane wa Oktoba 27, 2020 lilikwenda hoteli ya Aishi inayomilikiwa na Mbowe lakini ikiendeshwa na wawekezaji waUrusi wakimtafuta na Mbowe akaandika katika ukurasa wa Twitter:-  

“DC Sabaya akiwa na gari yenye namba za UN na silaha nzito za moto ameongoza genge la wahalifu kuvamia Hotel ya Kitalii ya Aishi, Machame kwa lengo la kunidhuru na kuniua. Wameteka, kutesa na kuumiza walinzi wawili wawili”

Katika tukio hilo, watu hao walipora silaha za walinzi hao na kuwatekeleza barabara ya Moshi-Arusha na hii ilimfanya Mbowe ashindwe kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu, akigombea ubunge, kwa kuhofia usalama wake.

Sabaya alipoulizwa na gazeti hili alikataa kuthibitisha au kukanusha uwepo wa tukio hilo akitaka Mbowe apuuzwe bila kufafanua CCTV zinazodaiwa kumuonyesha akiwa miongoni mwa wanaodaiwa kuvamia hoteli hiyo na silaha.



Mambo matano 2023

Akizungumza wakati wa ibada ya Shukrani na kuhamia katika nyumba yake hiyo iliyopo Machame Wilaya ya Hai, Mbowe alisema mwaka 2023 wataendelea kuhubiri haki katika taifa na kupigania usawa na ustawi wa wananchi wote.

"Ujumbe kwa watanzania ni kwamba yale ambayo tumekuwa tukiyahubiri kama chama kikuu cha upinzani waendelee kuyasimamia ikiwa ni pamoja na kupigania haki katika taifa, kupigania usawa na kupigania ustawi wa wananchi wote"

"Wajibu wetu wa kuendelea kudai katiba mpya pamoja na tume huru ya uchaguzi, itaendelea kuwa agenda ya chama chetu mwaka 2023 na tutatumia mbinu zote zinazowezekana chini ya jua kufanikisha azima hiyo,"alisisitiza Mbowe.

"Nawatakia watanzania wote mwisho mwema wa mwaka 2022 na tunapokwenda kuuanza 2023 ukawe mwaka wa matumaini na siyo mwaka wa kukata tamaa, mwaka wa kuhakikisha tunaongeza kasi katika kutengeneza misingi ya taifa letu”

“Misingi hii ndio itakayowezesha hatimaye kufanikisha yale ambayo tumekuwa tukipigania siku zote ambayo ni haki, demokrasia, ustawi wa wananchi wote viweze kupatikana kwa uhakika na kuipata Katiba mpya,"alisisitiza Mbowe.



Walichokisema Mbowe, Askofu Shoo

Akizungumzia nyumba ya ghorofa moja aliyohamia rasmi, Mbowe alisema ameianza kuijenga mwaka 2017 ambapo amepitia maumivu na machungu mengi wakati wa kuikamilisha lakini Mungu amewafanikisha.

"Leo imekuwa siku ya baraka kwangu na familia yangu ambapo tunahamia makazi yetu mapya ya kijijini, nyumba hii nilianza kuijenga April mwaka 2017 na katika kipindi hicho hadi leo nimekuwa gerezani kwa vipindi vitatu tofauti,”alisema.

Mbowe ambaye amekuwa Mbunge wa Hai kwa vipindi vitatu, alisema vipindi hivyo vitatu ukivichanganya vinakuwa ni mwaka mmoja na mwezi mmoja na amekuwa uhamishoni nchi za nje kwa zaidi ya miezi mitano.

"Lakini hatimaye pamoja na changamoto hizo namshukuru Mungu bado anaendelea kunijalia ujasiri na uthubutu wa kufanya kile ambacho nilikianza, safari hii imekuwa ni ndefu yenye maumivu na nimepitia nambo mengi Lakini namshukuru Mungu ukuu wake umeonekana," alisema Mbowe.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), AskofuFredrick Shoo, alisema hapo Mbowe na familia yake walipofika ni mkono wa Mungu, hivyo waendelee kumtegemea na kumtumikia katika maisha yao yote.

"Kufika hapa ni mkono wa Mungu, kwani mlianza nyumba hii mwaka 2017 na tunatambua mambo mliyopitia hivyo leo kuifungua ni jambo la kumshukuru Mungu na siku zote muendekee kumtegemea,"alisema Askofu Shoo.

Mbowe ni miongoni mwa viongozi wa upinzani aliyepitia madhila mengi katika utawala wa awamu ya tano ikiwamo jengo la Billicans kuvunjwa, miundombinu ya umwagiliaji Machame kung’olewa na akaunti zake benki kufungwa

Post a Comment

0 Comments