MADIWANI ARUSHA WAMSHUKIA KAMA MWEWE MBUNGE GAMBO WAMTAKA AACHE UZUSHI,UONGO NA UMBEA


 Na Joseph Ngilisho,Arusha


Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamemtaka Mbunge ,Mrisho Gambo kuacha kutafuta umaarufu kwa kuzusha uongo na umbea kwa kuwatuhumu viongozi wa serikali kuwa wanataka kumuua ikiwemo,tuhuma za Madiwani kuwa wamehongwa viwanja bure katika mradi wa Bondeni City wakati sio kweli.


Mbali ya hilo Madiwani hao walisema kuwa kitendo cha Gambo kusema wameruhusu fedha za Jijini kutoka bila utaratibu ni kauli iliyowadhalilisha wao na Chama kwa ujumla hivyo  waliomba hatua kali za kinidhamu ndani ya Chama na serikali zichukuliwa dhidi ya Mbunge huyo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti , Diwani wa Kata ya Baraa,Jacob Mollel alisema tuhuma za Gambo ni za uongo ,uzushi na zenye lengo la kujitafutia umaarufu.


Mollel ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya fedha na Utawala alisema hakuna pesa ya Halmashauri inalipwa bila kamati hiyo kuidhinisha na kwenda katika Baraza la Madiwani na Gambo ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.


Alisema Gambo amewavua nguo madiwani na Chama Cha Mapinduzi{CCM} na serikali ya Mkoaa wa Arusha  kwa kusema uongo hivyo hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine.


Diwani huyo alisema mradi wa Bondeni City ulipitishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani katika kikao cha novemba 22 mwaka huu kwa kupiga kura na hakuna diwani aliyepinga kati ya madiwani 33 waliohudhuria kikao hicho hivyo maamuzi yalikuwa halali kwa mujibu wa taratibu za vikao.


Alisema kuwa madai ya kusema madiwani wamepewa viwanja katika eneo hilo sio ya kweli na kama diwani amepewa basi alipewa kama mtu mwingine na sio kivuli cha udiwani kama anavyodai.

Naye Diwani wa Kata ya Ngarenaro,Issaya Doita ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya fedha na Utawala yeye alisema kauli ya Gambo ni kujitukana yeye mwenyewe kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Baraza la Madiwani na Mjumbe wa kamati ya fedha na Utawala.

Doita alisema kamati ya fedha na Utawala hukutana kila mwezi kupitisha bajeti na mambo mengine muhimu ya Jiji la Gambo ni mjumbe na kamati hiyo iliidhinisha fedha shilingi milioni 100 bila kufuata utaratibu sakata hilo haliwezi kumwacha salama.


Alisema Waziri Mkuu Kassimu Majawali aliwahi kuagiza tuhuma ambazo ziko kwa Mkaguzzi Mkuu wa Serikali{CAG} zinapaswa kuchukuliwa hatua na kama tuhuma anazodai ziko mezani asubiri utekelezaji na sio kuwahimiza kufanya mambo anayoyataka yeye.


Diwani Doita alisema Gambo hana mahusiano mazuri na  Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha,hana Mahusiano na Madiwani na hata sasa hana uhusiano Mazuri na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na Gambo anakuwa kama Mbunge wa Upinzani kila kukicha Nongwa.


Alisema utendaji kazi wa Mbunge Gambo ni wa kusikitisha na wa kushangaza kwani ni utendaji wa kuviziana kama paka anavyovizia panya na anafanya kazi kivyake vyake kwa kuwavizia watendaji wa Jiji wakosee ili aweze kusema nje ya vikao na sio ndani ya kikao.


Doita alisema Madiwani toka wamechaguliwa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hawajawahi kukaa na kupanga mipango ya maendeleo na hiyo yote inatokana na kutokuwa na mahusiano kati ya madiwani na Mbunge.


Naye Diwani wa Kata ya Lemara Naboth Silasile  yeye alisema kauli ya Gambo dhidi ya madiwani na watendaji wa Jiji ni uzushi,uongo,uchonganishi zenye lengo la kujitafutia umaarufu.


Silasile alisema sifa ya kiongozi bora kwanza huanza kuuliza tuhuma za ufisadi katika vikao lakini hilo kwa Gambo halipo wala hataki kuhudhuria vikao na kibaya zaidi unakwenda jukwaani katika mkutano wa Hadhara kusema uongo dhidi ya madiwani walio ndani ya Chama chako na kusema kuwa hilo halipaswi kuvumiliwa.


Alisema hakuna Diwani aliyepewa kiwanja cha bure katika Mradi wa Bondeni City kwa kivuli cha Udiwani na kama ana uthibitisho kwa tuhuma alizozitoa asisite kutoa hadharani ili hatua zichukuliwe.


Alisema eneo hilo limepimwa kisheria na halina kificho na kama kuna mtu amepewa kama raia mwingine yeye hawezi kulisemea na ila anapinga madiwani kupewa viwanja bure kwa kuwa ni uongo.


Ends....

Post a Comment

0 Comments