Na Joseph Ngilisho ARUSHA
SAKATA la wazazi katika shule ya msingi Msasani iliyopo jiji la Arusha,kuandamana wakipinga kuhamishwa kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo,Ridhiwan Ridhiwan ,limechukua sura mpya mara baada ya kaimu mkurugenzi wa jiji hilo kuibuka na kuwataka wazazi hao kufika ofisini kwake ili kupata ufafanuzi zaidi.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amepigilia msumari wa moto akidai kuwa mtumishi wa umma anawajibu wa kufanyakazi popote ,hivyo mabadiliko hayo yanalenga kuteta ufanisi zaidi wa kitaaluma na maendeleo.
Mapema wiki hii makumi ya wazazi , wengi wao wakiwa wanawake, waliandaa maandamano yasiyo rasimi katika shule hiyo wakitaka mwalimu huyo maarufu kwa ukanda huo ambaye amehamishiwa shule ya msingi Arusha(Arusha School) arejeshwe, shuleni hapo.
Mkurugenzi wa jiji la Arusha,Hargeney Chitukuro alifafanua kuwa uhamisho wa mwalimu Ridhiwani ni wa kawaida na yeye kama mtumishi wa umma anawajibu wa kufanyakazi mahala popote hapa nchini.
"Niwaomba hao wazazi au viongozi waje ofisini badala ya kuhamasisha maandamano na vurugu ,waje ofisini tuzungumze niwape ufafanuzi"alisema.
Chitukuro aliwatoa hofu wazazi hao kuwa mwalimu mkuu aliyechukua nafasi ya mwalimu Ridhiwani ni mzuri na anaimani ataendeleza vizuri misingi ya taaluma iliyo achwa na mwalimu Ridhiwani na mabadiliko hayo yamejikita kukuza taaluma na maendeleo kwa wanafunzi wa jiji la Arusha.
"Kimsingi niwatoe hofu wazazi mkuu huyo wa shule ni mwalimu mzuri na amefanyakazi nzuri Msasani ,tuliona kuwa shule ya Arusha ni shule kubwa na kongwe ila inachangamoto ya kiuongozi,hivyo Ridhiwani anauwezo wa kuondoa hizo changamoto"alisema
Aliongeza kuwa mwalimu aliyehamishiwa Msasani ni mtu mzuri ndio maana tumepeleka sh, milioni 480 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ya gorofa , tunaimani chini ya mkuu huyo mpya na makamu wake pamoja na kamati ya shule hakuna kitakachoharibika,niwaombe wazazi watoe ushirikiano.
"Mwalimu niliyempeleka Msasani nimefanya utafiti na kujiridhisha kuwa ni mwalimu mzuri, atawasaidia najua kuwa eneo hilo lina watu wengi na wanafunzi wengi lengo letu tunataka kuiimarisha Msasani ,huu ni utumishi wa umma mwalimu Ridhiwani hana kosa lolote ila ni uhamisho wa kawaida"
0 Comments