BY NGILISHO TV
Diwani wa Buzilasoga (CCM), David Shilinde na watu wengine 13 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Getruda Dotto.
Mbali na diwani huyo, yumo pia Mwenyekiti wa CCM Kijiji cha Ikoni B, William Nengo pamoja na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Tiluloza Alphonce.
Kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2022 imetajwa leo Desemba 6 na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Theophilius Lucas, akisema upelelezi bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo hakimu aanayesikiliza kesi hiyo, Tumsifu Barnabas ameaihirisha kesi hiyo hadi Desemba 20, 2022 huku washtakiwa wakirudishwa rumande katika gereza la Kasungamile.
Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo na umri wao kwenye mabano ni, Dilili Wali (60), Emmanuel Makala (33), Mkili Wali (48), Zacharia Meshack (44), Msafiri Jonas (38), Faustine Masweda (49), Anthony Method (24), Peter Lucas (29) na James Mazengo (30) na mtoto Yusuph Saimon (16)
Inadaiwa kuwa mnamo Novemba 5, 2022 katika Kitongoji cha Ikoni B, wilayani humo, mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Getruda Dotto akiwa nyumbani kwake ghafla alivamiwa na kundi la watu wakiwemo viongozi hao wakaanza kumshambulia kwa kutumia fimbo na marungu wakimtuhumu kuiba mihogo kwenye shamba la mwanakijiji mwenzake.
Inaelezwa kuwa mwanamke huyo alijaribu kujiteteana kusema shamba hilo aliachiwa na marehemu mume wake, lakini watu hao waliendelea kumshambulia na baadae wakamchoma moto na kusababisha kifo chake.
0 Comments