Na Joseph Ngilisho, Arusha
Sakata la mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo kutoa madai mazito ya kutishiwa kuuawa na watu aliodai ni viongozi wa serikali, limechukua sura mpya mara baada ya mkuu wa wilaya ya Arusha,Saidi Mtanda kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo kufika ofisini kwake
"Kama alitishiwa maisha kwanini hakutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ,kama unatuhuma yoyote unatakiwa wewe mwenye ukathibitishe kwenye vyombo vya usalama"
Akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake Mtanda alidai kutokuwa na taarifa za mbunge huyo kutaka kuuawa akisisitiza kuwa taarifa hizo hana na wilaya ya Arusha ipo salama .
Hata hivyo Mtanda alimshangaa Gambo ambaye amepakana naye kiofisi , kutompa taarifa hizo nzito akidai hata Dodoma walikuwa pamoja lakini hakumwambia chochote badala yake taarifa hizo anazisikia kupitia vyombo vya habari.
Siku chache zilizopita Gambo akihutubia mkutano wa hadhara eneo la soko kuu jijini hapa,alitamka pasipo kupepesa macho kuwa ,amevamiwa mara mbili nyumbani kwake na kuna watu wanamwinda wamuue na baadhi yao anawafahamu ni viongozi wa serikali.
Hata hivyo Gambo alisema watu hao wamekuwa wakimwinda ili wamuue kwa sumu lakini wameshindwa kwa sababu yeye sio mtu wa kula ovyo ovyo labda wamvamie getini wampige risasi ,tuhuma ambazo ni nzito.
0 Comments