MFANYABIASHARA WA MADINI AMTWANGA RISASI MTOZA USHURUWA MAGARI NI BAADA YA KUMDAI 7500 YA PARKING


BY NGILISHO NEWS .


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mchimbaji na mnunuzi wa madini, Ezekiel Luhwesha (31) kwa tuhuma za mauaji ya wakala wa maegesho ya magari, William Mgaya (58).


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 26, 2022, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema Luhwesha ambaye ni mkazi wa Matundasi Wilaya ya Chunya anatuhumiwa kufanya mauaji hayo kwa kumpiga Mgaya risasi.


Amesema kuwa tukio hilo limetokea maeneo ya Mafiati jijini Mbeya katika ofisi ya Tarura ambapo Mgaya akiwa na mwenzake Almas Shaban (32) wakikusanya ushuru walimkamata mtuhumiwa huyo baada ya ku-scan namba yake ya gari na kugundua kuwa lina deni la Sh7,500.


"Mtuhumiwa alitakiwa kulipa deni hilo lakini alihitaji kuona hilo deni linatokana na maegesho gani, hivyo kulazimika kuongozana naye hadi zilipo ofisi za Tarura kwa ajili kuangalia kwenye mfumo ili kupata taarifa za deni hilo,


"Mtuhumiwa alionyeshwa taarifa za deni hilo na kuridhika kuahidi kulipa deni hilo lakini wakala (Mgaya) alimtaka kulipa deni hilo papo hapo kutokana na deni hilo kuwa la muda mrefu” amesema


Kamanda Kuzaga amesema kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutakiwa kulipa deni hilo kulitokea majibizano hali iliyopelekea mtuhumiwa kutoa bastola na kufyatua risasi moja uelekeo alipokuwa Mgaya na kumpiga sehemu ya kifuani.


Amesema baada ya kufwatuliwa risasi, Mgaya alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.


Kamanda Kuzaga anatoa wito kwa wanaomiliki silaha kuzingatia masharti ya umilikishwaji wa silaha hizo.

Post a Comment

0 Comments