Na Joseph Ngilisho Arusha
WANACHAMA wa chama cha wakulima Tanganyika TFA, wamelalamikia kutonufaika na chama hicho tangu kianzishwe mwaka 1935 ikiwemo kutopata gawio kulingana na fedha walizowekeza huku baadhi ya wazee wakifariki dunia.
Wakiongea kwa uchungu katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika makao makuu ya TFA jijini Arusha ulioenda sanjari na uchaguzi wa bodi ya wakurugenzi.
Wanachama hao wameiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru mkoani hapa kuchunguza mwenendo wa chama hicho ikiweno mikataba ya upangishwaji wakidai kwamba chama hicho kina vitega uchumi vingi ikiwemo biashara ya pembejeo na nyumba za upangizaji lakini haviwanufaishi.
Akiongea katika mkutano huo mmoja ya mwanachana,Bonface Mollel alisema haoni manufaa ya chama hicho licha ya kuongezeka kwa mapato yanayofikia kiasi cha sh,bilioni 12 kwa mwaka lakini fedha hizo hazionekani .
Alisema usiri wa mikataba ya upangishaji wa majengo ya TFA pamoja na matumizi makubwa yanayofanywa na bodi ya wakurugenzi yanayofikia sh,milioni 65 kwa mwaka ni sehemu ya ulaji mkubwa wa mapato ya TFA.
Mollel alitolea mfano kuwa baba yake mzazi aitwaye Lobikeki oloitai mwenye umri wa miaka 105, mkazi wa Ngaramtoni alikuwa mwanachama mwaanzilishi wa TFA lakini hadi sasa ameamua kupumzika hajawahi kupata gawio lolote.
"Ndani ya TFA kuna mchwa ndani ya mchwa wanatafuna mapato ukizingatia kuwa TFA ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo magodauni ya kupangisha ,maduka ya pembejeo ambapo mapato yakikusanywa yanafukia bilioni 12. Kwa mwaka fedha ambazo hatujui zinaenda wapi"
Mkulima mwingine Godfrey Lyiru kutoka Akeri Wilaya ya Arumeru alisema kuwa kila mwaka wanapofanya mkutano mkuu wamekuwa wakipewa makabrasha yaliyoandikwa kitaalamu na wazee ambao wengi wao wamepoteza hata uwezo wa kuona vizuri wanaambulia patupu na wanapohoji wanaambiwa wakasome makabrasha.
"Kila tukifanya uchaguzi viongozi wanarudi wale wale na mbaya zaidi wamejiwekea kampuni yao ya mahesabu ya auditing ambayo sisi kama wanachama hatuna imani nayo,sisi tunaomba Takukuru waje wachunguze"
Alisema kila mwaka wanapofanya uchaguzi wamekuwa wakiambulia chakula cha kugombania na posho ya sh, elfu 50 jambo alilosema ni udhalilishaji kwa wazee wenye umri mkubwa ambao husafiri umbali mrefu kuja kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi mtendaji wa TFA, Justine Shirima alikiri chama hicho kutotoa gawio kwa wanachama wake tangia kuanzishwa mwaka 1935 akidai kwamba tatizo lilitokana na uendeshaji kwa viongozi waliopita.
"Katika kipindi chote cha uendeshaji tangia TFA ianzishwe mwaka 1935 ,chama kimekuwa kikipitia changamoto ya kutotengeneza faida na kwa mujibu wa taratibu za makampuni ili ulipe gawio inapaswa uwe umetengeneza faida"alisema
Shirima ambaye anamiaka 7 tangia akabidhiwe mamlaka ya kuendesha chama hicho alisema kuwa kwa sasa chama hicho kimetengeneza faida ila haijafikia kulipa gawio kwa wanachama.
Alisema kuwa hadi mwishoni mwa mwaka huu TFA imeweza kufikisha mauzo yanayofikia kiasi cha sh, 12.9 kutoka sh,bilioni 4 ya mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 89.
Alisema matarajio ni kukuza biashara hadi kufikia makusanyo ya sh,bilioni 22 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.
Alivitaja baadhi ya vitega uchumi ambavyo TFA inafanya biashara kuwa ni pamoja na biashara ya pembejeo,upangishaji wa majengo na matarajio ni kuanza kununua mazao toka kwa wakulima na wanahisa pamoja na kuanzisha kilimo cha mbegu.
Mkutano huo pia ulifanya uchaguzi wa bodi ya wakurugenzi watano na kufanikiwa kumrejesha aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Sirikwa ambaye alichaguliwa kwa kishindo.
Ends..
0 Comments