CHADEMA ARUSHA YACHARUKA, YAONYA VIKALI SERIKALI


Na Joseph Ngilisho Arusha 

BARAZA la wazee la chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) BAWACHA, mkoa wa Arusha,limeunga mkono tamko la katibu mkuu wa chama hicho Taifa kupinga ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu na kusema kuwa kikosi hicho kimeshindwa kukidhi mahitaji ya wananchi kuhusu demokrasia na katiba mpya.

Mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Arusha,Emmanuel  Zachary maarufu kwa jina la Baba Bony,alisema wanaungana na katibu wao Taifa, John Mnyika ambaye alisema kuwa kikosi kazi hicho kiliundwa ili kuchelewesha mchakati wa katiba mpya na kutumia fedha  nyingi wakati kazi ya kutafuta maoni ya wananchi ilifanywa na Tume ya mabadiliko ya katiba ikiongozwa na jaji Joseph Warioba.


Mwenyekiti huyo alisema kuwa tume hiyo haikuwakilisha wananchi bali ililenga kusafisha njia ya mgombea urais wa ccm ifikapo mwaka 2025.

Alisema kuwa wazee wa chadema mkoa wa Arusha kwa sasa wanataka mabadiliko ya kweli kwa kupata katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ili kupata viongozi na sio watawala .

"Wazee wa Chadema tumekusanyika hapa kuunga mkono kauli ya katibu mkuu John Mnyika kuwa hatukubaliani na kikosi kazi cha rais samia ,kwanza pesa zilizotumia ni ufujaji wa fedha za wananchi na ukitafakari ni longolongo za kuchelewesha mchakato wa katiba mpya"
Baba Bonny alitahadhalisha matumizi mabaya ya fedha za wananchi na kutaka kikosi kazi hicho kujiandaa kuzitapika kwa sababu  fedha hizo ni jasho la wananchi na walipewa kimakosa 

Alisema wazee hawezi kuona fedha za umma zikichezewa na kukaa kimya wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma muhimu wakati fedha nyingi zinapelekwa kwenye matumizi yasiyona tija.

"Tunachotaka kwa sasa ni katiba mpya ndio itakuwa mwarobaini wa demokrasia  hapa nchini,hayo mambo yaliyopendekezwa na hicho kikosi kazi mbona hayafanyiwi kazi ikiwemo kuruhusu mkutano ya hadhara"

Wakati huo huo ,mwenyekiti  huyo aliitumpia lawama ofisi ya msajiri wa vyama vya siasa nchini na kusema kuwa ofisi hiyo inatumika kama rungu la kuvipiga vyama vya upinzani nchini hususani chadema.

"Tunamwonya msajiri wa vyama vya siasa nchini kuacha kutumika kama rungu la ccm kuvipiga vyama vya upinzani "

Katika hatua nyingine wazee hao wa Chadema mkoani hapa,wamempongeza mwenyekiti wao wa  taifa,Freeman Mbowe kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), katika mkutano mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika  Novemba 9 mwaka huu.

Mmoja ya wanachama wa baraza hilo ,Bakari Chapa alisema hatua ya Mbowe kuchaguliwa kumeiheshimisha chadema na taifa la Tanzania na  inaonesha uimara wa chadema na kuwataka wanachadema kutembea kifua mbele kwa kujivunia nafasi hiyo nyeti aliyopewa kiongozi wao.

"Mbowe anauwezo wa kulinda demokrasia duniani hivyo hatua hii ni mwanzo wa kudai kwa nguvu katiba mpya hapq nchini"

Naye mwenyekiti wa Chadema babati vijijini ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika kikao hicho, Pauline Nasisi aliwataka wanachadema kutokuwa waoga katika mapambano ya katiba mpya kwa sababu taifa hili haliendi bila kelele za wananchi.

"Jambo ninaloweza kusisitiza hapa wananchi  tupambane katika kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi pia wanawake chadema tujitokeze kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani,ubunge na nafasi zingine za juu za chama"

Ends...












Post a Comment

0 Comments