Na Joseph Ngilisho ,ARUSHA
WATU wasiofahamika wamevunja kitasa cha gari aina ya Prado na kupora sh,milioni 7, fedha za mishahara ya wafanyakazi baada ya mmiliki wa gari hilo Zephania Kwayu kutoka kuchukua fedha hizo benki.
Tukio hilo limetokea mapema leo majira ya saa 3 asubuhi kando na benki ya NBC barabara ya uhuru jijini Arusha wakati fedha hizo zikiwa kwenye gari hilo lenye namba T 694 BAB lililokuwa limeegeshwa eneo hilo jirani na Kanisa Katoliki la Mt.Thereza ambako hivi karibuni gari la Padri lilivunjwa kioo na majambazi na kujaribu kupora mamilioni ya fedha zikitoka benki.
Akiongea mara baada ya tukio hili ,Kwayu ambaye anamiliki kampuni ya ukandarasi jijini hapa,alisema kuwa asubuhi alienda benki kwa ajili ya kuchukua fedha za mishahara ya wafanyakazi wake.
Alisema mara baada ya kutoka benki alienda kuegesha gari lake eneo hilo na kwenda ofisi cha kampuni ya simu ya Vodacom kwa ajili ya kurejesha line yake ya simu iliyokuwa imeharibika.
Alisema wakati anarudi na kujaribu kuingiza funguo kwenye kitasa cha gari lake ndipo alipobaini kwamba kimevunjwa.
"Niliingia ndani ya gari kuangalia fedha kwenye droo ya gari na kukuta droo ipo wazi na fedha hazipo nilichanganikiwa nisijue la kufanya kwani zilikuwa ni fedha za mishahara ya wafanyakazi"
"Nahisi watu hao walinifuatilia tangia nikiwa benki hadi nilipokuja kuegesha gari eneo hili la tukio"alisema Kwayu huku akilengwalengwa na machozi
Alisema mara baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa polisi waliokuwa wakilinda benki ya NBC ambao waliwasiliana na wenzao ambao walifika na kushuhudia tukio .
Mashuhuda wa tukio hilo ambao ni kina mama wanaouza maua eneo hilo ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walisema waliona mtu akifika kwenye gari hilo ila hawakufahamu kama alikuwa ni mhalifu .
"Tulimwona mtu mmoja akijaribu kufungua mlango wa dereva ila sikujua kama alikuwa ni mwizi na baadaye aliondoka "
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku mbili zimepita majambazi wengine kuvunja gari ya Padri na kujaribu kupora mamilioni ya fedha baada ya padri kutoka benki kuchukua fedha hizo.
Kamanda wa polisi Mkoani Arusha Justine Masejo hakuweza kupatikana ofisini kuzungumzia tukio hilo.
Ends..
0 Comments