UTEUZI :RAIS SAMIA AFANYA TEUZI KIBAO ,AMPIGA CHINI MGANGA MKUU WA SERIKALI KUPANGIWA KAZI NYINGINE


 BY NGILISHO TV Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi wawili pamoja na wajumbe wa bodi hizo.


Pia, amewateua watendaji watatu wa serikali na taasisi za umma akiwemo Mganga Mkuu wa Serikali.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 22, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia amemteua katibu Mkuu mstaafu, Dk Florens Turuka kuwa mwenyekiti wa bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka .

Pia, Rais Samia amewateua maofisa watano kuwa wajumbe wa bodi hiyo, wajumbe hao ni Zainab Msimbe (Mhasibu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Johansen Kahatano (Mkurugenzi wa Barabara - Latra) na Aron Kisaka (Mkurugenzi wa Huduma za Usafirishaji, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi).


Wengine ni Benjamin Kiloba (Mkurugenzi wa Miundombinu – Mamlaka ya Serikali Mtandao) na Mwantumu Mshirazi Salim (Katibu wa Kampuni, Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Dar es Salaam – EPZA).


Taarifa hiyo imebainisha kwamba Rais Samia amemteua Beng’i Issa ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), kuwa mwenyekiti wa bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa.


Wajumbe wa bodi hiyo walioteuliwa ni pamoja na Dk Hemed Mpili (Ofisa Ugavi Mwandamizi – Tamisemi), Profesa Provident Dimoso (Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini) na Said Panga (Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu – Chuo cha Mipango).


Wengine ni Joseph Chilambo (Meneja Uwezeshaji Biashara, Benki ya Maendeleo – TIB) na John Mihayo Cheyo (Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Ofisi ya Rais).


Kwa upande wa watendaji, taarifa hiyo imebainisha kwamba Rais Samia amemteua Profesa Tumaini Nagu kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Dk Aifelo Sichalwe ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Post a Comment

0 Comments