BY NGILISHO,NEWS
Wakati Kamanda wa Majeshi ya Nchi Kavu wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba akisakamwa kwa andiko lake kuwa atahitaji wiki mbili kuliteka jiji la Nairobi lililopo nchini Kenya, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amempandisha cheo kutoka Luteni Jenerali kuwa Jenerali.
Kampala. Wakati Kamanda wa Majeshi ya Nchi Kavu wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba akisakamwa kwa andiko lake kuwa atahitaji wiki mbili kuliteka jiji la Nairobi lililopo nchini Kenya, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amempandisha cheo kutoka Luteni Jenerali kuwa Jenerali.
Hatua hiyo ya Rais Museveni imekuja saa chache baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda kuweka wazi kuwa haifanyi kazi kupitia mitandao ya kijamii na inaheshimu na kuthamini uhusiano wake na Kenya.
Jenerali Muhoozi ni mtoto wa Rais Museveni, ambaye kila kukicha amekuwa akiandika mambo yanayozua mjadala, kuzusha hofu na mengine kuweka
Juzi aliandika kwamba atahitaji wiki mbili pekee yeye na jeshi lake kuliteka jiji la Nairobi.
Hoja hiyo ilizusha mjadala mkubwa ambapo baadhi ya watu waliita kuwa ni fedheha ya kidiplomasia, lakini pia itasababisha mikwaruzano kwa majirani hao.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilitoa waraka ikisema wanathamini uhusiano thabiti uliopo kati ya Kenya na Uganda kwa kuzingatia historia ya kuishi pamoja, kuheshimiana, kuaminiana na nia ya kujenga Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye umoja.
“Serikali ya Jamhuri ya Uganda haitekelezi sera yake ya mambo ya nje na shughuli nyingine rasmi kupitia mitandao ya kijamii wala haitegemei vyanzo vya mitandao ya kijamii katika kushughulikia Serikali nyingine huru,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Amlaumu Kenyatta
Jenerali Muhoozi, katika andiko lake alianza kwa kumlaumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye anamtaja kama “kaka yake mkubwa”, kwa kutowania muhula wa tatu katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022, akiongeza kuwa rais huyo mstaafu angeshinda uchaguzi kwa urahisi iwapo angegombea kwa muhula mwingine wa tatu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kenya, Rais anaruhusiwa kugombea mihula miwili tu ya vipindi vya miaka mitano, na kwa sababu hiyo hangeweza kugombea muhula wa tatu isipokuwa katiba ibadilishwe kwanza.
Lakini Muhoozi, 48, anapendekeza Kenyatta, ambaye alikabidhi madaraka kwa Rais William Ruto Septemba 13, 2022, angeweza kubadilisha Katiba ili kusalia madarakani. “Haha! Nawapenda jamaa zangu wa Kenya. Katiba? Utawala wa sheria? Lazima uwe unatania! Kwetu (Uganda), kuna mapinduzi tu na muda si mrefu mtayafahamu!”
Isitoshe, Muhoozi alidai kwa hisia kwamba anahitaji wiki mbili ili kupindua serikali ya Rais Ruto.
Mabadiliko
Jenerali ndicho cheo cha juu zaidi katika uongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda.
Kabla ya Rais Museveni kutangaza mabadiliko hayo, Muhoozi aliandika “Nilikuwa na mazungumzo mazuri na baba yangu asubuhi ya leo. Inavyoonekana, tweets zangu ziliwaogopesha Wakenya kupita kiasi. Atatangaza mabadiliko. Kuna maombi maalumu nitafanya kwa ajili ya jeshi letu,” alitweet.
Kuikamata Nairobi
“Haitatuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki mbili kuikamata Nairobi,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Aliendelea kuandika: “Nina furaha kwamba wanachama wa wilaya yetu nchini Kenya, wamejibu kwa shauku kwenye ‘tweet’ yangu. Bado ni wiki mbili kufika Nairobi! Baada ya jeshi letu kuiteka Nairobi, nitaishi wapi? Westlands? Riverside?” Haikuweza kufahamika mara moja iwapo ni yeye mwenyewe alikuwa akiisimamia akaunti yake ya Twitter au la. Kwa bahati mbaya, Rais Museveni, 78, amefaidika mara mbili kutokana na mabadiliko ya Katiba ya kuitawala Uganda kwa takriban miongo minne. Hii ni pamoja na hatua ya kuondoa mihula na ukomo wa umri kwenye katiba.
Muhoozi pia amemkashifu kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, akisema kamwe hatatawala Uganda.
“Kabobi anapaswa kujua kwamba hatutamruhusu kamwe kuwa Rais wa nchi hii!” aliandika Muhoozi.
Muhoozi mwenye utata ameibuka kuwa kipenzi cha kumrithi baba yake iwapo ataamua kustaafu.
Bobi Wine alishindana na Museveni katika uchaguzi wa mwaka 2021 na kuibuka wa pili, Alipinga matokeo katika Mahakama ya Juu lakini baadaye akaiondoa kesi.
Ltuteni Jenerali Kainerugaba aliyezaliwa Aprili 24, 1974 jijin Dar es Salaam, Tanzania, kwa sasa ni kamanda wa jeshi la Uganda akihudumu kama kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya UPDF na ambaye hapo awali alikuwa kamanda wa Kikosi Maalumu SFC ambavyo vyote, UPDF na SFC, vinashutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi na utekaji nyara. Muhoozi na maafisa wengine wakuu wametajwa katika malalamiko ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Mwaka 2017 Muhoozi aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, na hivyo kuchochea uvumi kuwa anatayarishwa kwa urais.
Akiwa amejulikana hapo awali kuwa mfuatiliaji wa kimya kimya katika siasa za Uganda, Muhoozi hivi karibuni ameingia kwenye mtandao wa twitter ghafla akizungumzia masuala kadhaa ya kijamii na kisiasa nchini Uganda lakini hasa akiisifu UPDF ambayo anaisifu kama ‘Jeshi kubwa zaidi Dunia’.
Katika hotuba ya 2013 kwa Uongozi Mkuu wa UPDF, Rais Museveni alisema: “Nimefurahishwa sana kwamba Muhoozi amegeuka kuwa afisa makini sana, mtulivu na aliyejitolea katika ujenzi wa jeshi” akimaanisha kazi ya Muhoozi katika kujenga Kamandi ya Kikosi Maalumu.
Muhoozi amepewa jina na baadhi ya vyombo vya habari kama ‘Jenerali wa kutweet’, wakimaanisha matumizi yake makubwa ya ghafla ya Twitter, mara kwa mara akichapisha maudhui ambayo wengine hawaoni kuwa yanamfaa mtu wa wadhifa na cheo chake katika Jeshi na katika nyanja ya kijamii ya Uganda.
0 Comments