WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema sekta ya utalii hapa nchini imezidi kuimarika na takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kuwa watalii wanaokuja Tanzania wameongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 na kufikia watalii 922,692 mwaka 2021.
Majaliwa ameyasema hayo mapema leo jijini Arusha,wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani – Kamisheni ya Afrika, unaohudhuliwa na nchi 33 wanachama.
Alisema kuwa mbali na ongezeko hilo la watalii, pia mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021.
“Pia takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa Sekta ya Utalii inazidi kuimarika zaidi hususan baada ya uzinduzi wa Programu Maalumu iliyotekelezwa na Mheshimiwa Rais Samia ya The Roya Tour iliyozinduliwa rasmi Aprili 2022 katika soko letu la utalii la kimkakati nchini Marekani.”
Alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mwongozo mzuri uliotolewa na Shirika la Utalii Duniani kwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania katika kukabiliana na athari za UVIKO – 19.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuendelea kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
Majaliwa alitoa rai kwa mashirika na taasisi za kimataifa kuendelea kuiamini Tanzania na kuichagua kama sehemu sahihi ya kufanyia shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano adhimu kama hii.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani, Zurab Pololikashvili amesema kuwa baada ya mlipuko wa janga la UVIKO 19 nchi nyingi duniani ziliathirika kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii, hivyo watahakikisha wanaendelea kuweka mikakati ya kurejesha sekta hiyo katika hali yake ya kawaida.
Alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina vivutio bora vya kutembelea kwa ajili ya utalii na watu wengi duniani wameitambua kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi yetu pamoja na jumuiya ya Kimataifa katika masuala mbalimbali yakiwemo ya utalii.
Ends....
0 Comments