KIWANDA CHA PEPSI MATATANI KWA KUKWEPA KODI ,GARI LAKE LA SODA LASHIKILIWA LONGIDO

Na Joseph Ngilisho Arusha 

HALMASHAURI ya  wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha ,inalishikilia gari la Mauzo la kampuni ya Vinywaji baridi ya Pepsi (SBC)ya jijini Arusha baada ya kampuni hiyo kukwepa kodi kwa kipindi cha miaka 7.

Akiongea na Gazeti hili mhasibu mkuu wa halmashauri hiyo,Magige Chacha alisema kuwa gari hilo aina Eicher lenye namba za usajiri T 894 DSH lilikamatwa jana majira ya jioni ambalo bado linashikiliwa katika halmashauri hiyo.


Chacha alisema kuwa kampuni hiyo ya Pepsi ya jijini Arusha kwa muda mrefu wamekaidi kulipa kodi ya huduma(Service levy)katika wilaya hiyo licha ya uongozi kuwaandikia barua marakadhaa kwa njia ya  kawaida na barua pepe (email) lakini walikuwa wakipiga chenga na kudharau.

"Hii kampuni ya Pepsi ni wasumbufu sana hawajatulipa kwa zaidi ya miaka sita au saba , kila tukijaribu kuwatafuta wanatupiga chenga tukaamua kuwandikia demand note lakini pia haikuzaa matunda ndio maana jana tukaamua kukamata gari lao"

Alisema kuwa kampuni hiyo  ilipaswa kulipa kodi ya huduma 'service levy' kila baada ya miezi mitatu ,lakini katika kipindi cha miaka saba haikuwahi kulipa jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

'Baada ya kukamata gari lao viongozi wa kampuni hiyo walifika ofisini leo asubuhi na kutakiwa kulipa kodi hiyo baada ya kuleta mahesabu yao ya mauzo kutoka mamlaka ya mapato Tanzania TRA ambapo halimashauri hiyo huchukua asilimia 0.3 ya mauzo' 

Hadi gazeti hili linaondoka katika halimashauri hiyo gari hilo likiwa na shehena ya soda lilikuwa bado linashikiliwa katika ofisi za halimashauri  hiyo.

Kwa upande wake meneja Rasilimali watu wa kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina la Edwin Abogasti alisema kuwa hana taarifa za kushikiliwa kwa gari la kiwanda chao akidai kwamba halmashauri hiyo haiwadai chochote kwa kuwa wao ni walipa kodi wazuri.

"Sisi ni walipakodi wakubwa na ndio maana tulishawahi kuzawadiwa cheti na TRA na hizo taarifa za kushikiliwa kwa gari letu wewe ndio unaniambia"

Taarifa za ndani kutoka halmashauri hiyo zinadai kwamba majira ya asubuhi uongozi wa SBC kutoka jijini Arusha ulitua katika  halmashauri hiyo wakihaha kukomboa gari hilo lililokuwa limesheheni soda za mauzo.

Hata hivyo baadaye pande zote mbili waliingia kwenye kikao cha mazungumzo ili kuona namna bora ya kulipa deni hilo ambalo bado halikuwekwa wazi mpaka mahesabu ya mauzo yapatikane kutoka TRA.

Hata hivyo chacha aliongeza kuwa baada ya mazungumzo hayo,Kampuni hiyo imeonesha nia ya kulipa deni hilo na kuahidi  kila baada ya miezi mitatu watakuwa wanalipa kodi hiyo ya huduma bila usumbufu wowote.

Ends...


Post a Comment

0 Comments