Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imekwama kusikiliza kesi za uhujumu uchumi zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wanne baada ya mashahidi wa Jamhuri kutofika mahakamani .
Mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha katika halmashauri hiyo Mariam Mshana, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi, Innocent Maduhu, Alex Daniel na Nuru Ginana (aliyekuwa mchumi).
Leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 Mahakama hiyo ilipanga kuanza kusikiliza kesi mbili za uhujumu uchumi kati ya tatu kwa upande wa mashahidi wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule huku utetezi ukiwakilishwa na Mawakili Edmund Ngemela, Sabato Ngogo na Jacob Msigwa.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022, Wakili Janeth aliileza mahakama kuwa wanaomba tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo kufuatia mashahidi kutokuwepo mahakamani hapo huku wakisubiria hakimu wa kusikiliza kesi hiyo kama ilivyo elezwa katika hatua za awali.
Kesi zote mbili zimeahirishwa na zinatarajiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Novemba 8 hadi 10,mwaka huu.
Wakati huo huo kesi ya kujeruhi na kubaka namba 23ya mwaka 2022 inayomkabili mkazi wa Ketumbeine, Longido, Namendea Lesiria na mwenzake imeanza kuunguruma katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha.
Shahidi wa kwanza wa jamhuri ambaye ni binti wa miaka 15 Mesoni Kashiro aliyekuwa ameolewa na mtuhumiwa aliieleza mahakama kwa lugha ya kimasai kwamba mtuhumiwa na mwenzake ,septemba 13 mwaka huu walimshambulia kwa fimbo akiwa hana nguo na kisha kumfunga kamba kwenye mti na kumtelekeza porini kwa muda wa siku tatu bila kula wala kunywa .
Akiongea huku akibubujikwa na machozi aliieleza mahakama hiyo kwamba siku ya tatu alighunduliwa na vijana waliokuwa wakichunga mifugo ambao walimsaidia kufungua kamba na kmwacha katika mti huo akiwa hawezi kutembea.
Anasema simu iliyofuata alitokea mzee ambaye alimtambua na kumsaidia kumrejesha nyumbani akiwa na majeraha makubwa mwilini na kisha kumpeleka zahanati kwenye matibabu na baadaye kutoa taarifa polisi .
.
0 Comments