WANANCHI WAANDAMANA KUMKATAA BALOZI WA CCM,WADAI HAWAJAMCHAGUA ,ANAWALETEA MGAMBO KUWAKAMATA USIKU WA MANANE WAKIWA WAMELALA,YEYE AKANA ADAI NI WIVU TU

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA 

Wakazi zaidi ya 100 wa kitongoji cha Siwandeti ,kata ya Kiranyi wilaya ya Arumeru mkoani Arusha,wameandamana kumkataa balozi wao wa CCM,Christine Zakayo kwa madai kwamba hakutokana na chaguo lao na amekuwa akiwaletea migambo kuwabughudhi usiku wa manane wakiwa wamelala.

Wakiongea kwa jazba jana baada ya kujikusanya ofisi ya tawi la ccm,katika kitongoji hicho, wananchi hao,wamemlalamikia mwenyekiti wa kijiji hicho,Lawrence Meminyeki kwa madai ya kumkumbatia wakati anajua hakutokana na chaguo la wananchi wa kitongoji hicho. 
Aidha wananchi hao wamemtuhumu mwenyekiti wa kijiji hicho kuwa na mahusiano na balozi huyo wa nyumba kumi ndio maana balozi huyo amekuwa na kiburi cha kuwanyanyasa kwa kuwaletea migambo usiku wa manane ili kuwakamata wananchi wanaompinga na hivyo wamekitaka chama cha mapinduzi ccm kumwondoa mara moja balozi huyo kabla hawajajichukukua sheria mkononi.

Baadhi ya wakazi hao, Eva Michael alidai kwamba kitongoji chao hakina balozi hadi sasa na wao kama wananchi wanakosa uongozi wa karibu wa kuwasaidia, ila huyo anayejiita balozi ametengenezwa kimchongo na mwenyekiti wao wa kijiji.

"Sisi katika kitongoji chetu hatuna Balozi kabisa,tunakosa pa kupeleka shida zetu na huyo Christine  sisi hatumtambui  ni balozi wa mchongo aliyechaguliwa na mwenyekiti"alisema Eva.


Naye Vickta Mshangila alisema kitongoji chao kimekosa balozi kwa muda mrefu na hivyo wao kama wananchi kukosa pa kupeleka kero zao ikiwemo changamoto za maji na uhalifu mdogo mdogo.

Alisema kuwa hawamtambui balozi aliyekuwepo kwani ameteuliwa kinyemela bila kufanyika kwa uchaguzi ndio maana hana uchungu na wananchi wake na amekuwa akiwanyanyasa kwa kuwatumia migambo ili wakamatwe pale wanapompinga.

Awali mwenyekiti wa kijiji hicho cha Siwandeti ,Lawrence Meminyeki alifika kwenye mkusanyiko wa wananchi hao na kuwataka watawanyiki kwani hakuwa nantaarifa na madai yao ila anaowahitaji ofisini kwake ni wananchi 12 aliowatuhumu kuandamana usiku.

"Jamani mimi siwahitaji mjikusanye hapa ila ninaowahitaji kuongea nao ofisini ni wananchi 12 tu ambao waliandamana usiku"alisema.
Akizungumzia tuhuma za mahusiano na balozi huyo alidai jambo hilo halijui ila alisisitiza kuwa balozi huyo alichaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa kitongoji hicho.

 Naye mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi kata ya Kiranyi, James Kivuyo alipohojiwa juu ya uhalali wa balozi huyo alisema kuwa bado hajapata taarifa kamili ila kama kweli hakujaguliwa basi chama hakiwezi kumumilia hilo.

"Hilo sakata la wananchi kumkataa balozi 
wa ccm nimelisikia ila kama ni kweli chama hakiwezi kuvumilia ngoja nifuatilie nitakupatia taarifa"alisema.

Kwa upande wake Christine Zakayo, alisema sakata hilo limeibuka kutokana na wivu wa watu wachache baada ya mabalozi kulipwa posho katika zoezi la sensa.
Alisema yeye alichaguliwa kihalali  akiwa mgombea pekee aliyepigiwa kura za ndio na hapana baada ya mpinzani wake jina lake kutorudi na yeye kupata kura 38 za ndio huku kura tano zikimkataa.

'Hilo suala la mahusiano ya kimapenzi na mwenyekiti wa kijiji  ni uchafu unaoenezwa na wapinzani wangu kwa lengo la kunichafua na suala la wananchi kukamatwa na migambo usiku wa manane mimi silijui "alisema.

Hata hivyo alimtuhumu balozi aliyemaliza muda wake ambaye jina lake lilikatwa kuwa ndiye anayeratibu sakata hilo kwa maslahi yake.

Ends....



Post a Comment

0 Comments