Na Joseph Ngilisho Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linawashikilia watuhumiwa 38 wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu akiwemo dereva mmoja aliyekutwa akisafirisha kilo 390 za Mirungi kwa kuzipakia kwenye Lori la mafuta.
Alisema kati yao mmoja amekutwa akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kwa kutumia gari la kubeba mafuta.
Akitoa taarifa hiyo mapema leo ,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti .
Alisema kuwa Operesheni hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 05 hadi Septemba 10, 2022 na iliongozwa na Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha kwa lengo la kukabiliana na uhalifu ambao umeanza kutishia amani mkoani
hapa.
Kamanda Masejo alisema kuwa sep,10 mwaka huu majira ya saa 12:30 asubuhi katika kata ya Kikwe wilayani Arumeru, Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata,Allen Wilbard Kasamu (49) dereva na mkazi wa Suye Jijini Arusha akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilo 390.75
Alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akisafirisha madawa hizo kwa kutumia gari aina ya Mitsubish Canter – Tanker ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubeba mafuta,ambapo mtuhumiwa alipakia ndani ya tenki la mafuta ili asijulikane.
Katika operesheni hiyo jeshi hilo lilifanikiwa kukamata pikipiki 13 zilizokua zinatumika katika matukio ya uhalifu, gongo lita 08, bangi yenye uzito wa kilo 70 pamoja na laptop 03.
Hata hivyo Kamanda Masejo alisema kuwa hadi sasa jeshi la Polisi mkoani humo bado linaendelea na upelelezi ikiwemo kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutolewa maamuzi.
Alitoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Sambamba na hilo pia amewataka baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na uhalifu hususani biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani wataendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua.
Katika hatua nyingine Kamanda Masejo alisema kwa Mkoa wa Arusha wananchi wameanza kujitokeza kusalimisha silaha zao katika vituo vya polisi .
Alitoa rai kwa wanamiliki wa silaha wanaomiliki kinyume cha Sheria kufika katika vituo vya Polisi ama ofisi za watendaji wa mitaa kusalimisha silaha hizo katika kipindi hiki ambacho Serikali imetoa msamaha kwa ambao watasalimisha.
Ends.
0 Comments