MKAZI wa Kijiji cha Chekereni,Josephat January (75) maarufu kwa jina la Mparee anayedaiwa kuwa ni Mganga wa tiba za Kienyeji, ameteketea kwa moto kiasi cha kutotambulika ,uliozuka nyumbani kwake usiku wa manane akiwa usingizini amelala na kuteketeza kila kitu ikiwemo kuku,bata, Sungura na fedha huku mke na mtoto wake wakinusurika .
Shuhuda wa tukio hilo Peter Kivuyo alisema kuwa marehemu alikutwa na mauti wakati akijaribu kuokoa fedha zake zilizokuwa ndani ya nyumba yake baada ya moto huo kuibuka ghafla akiwa amelala .
Alisema moto huo ulizuka majira ya usiku huku chanzo kikiwa hakijulikani japo taarifa za awali zinaonesha kuwa umetokana na jiko la kuni kusahaulika kuzimwa.
Alisema kuwa nyumba ya marehemu iliyokuwa imejengwa kwa mifuko ya nailoni ilishika moto, uliokolezwa na upepo na kuteketeza kila kitu zikiwepo fedha alizokuwa amehifadhi marehemu baada ya kuuza magunia zaidi ya 20 ya mahindi.
Alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alielekea eneo la tukio na kukuta baadhi ya wananchi wakijaribu kuuzima moto huo kabla ya gari la zima moto kufika ,hata hivyo moto ulikuwa mkali uliowashinda nguvu na kuteketeza kila kitu.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Chekereni, Eliasi Lesembu alisema kuwa alipata taarifa za tukio hilo jana majira ya saa 4 usiku na kutoa taarifa kwa kikosi cha uokozi na zima moto.
Alisema mara baada ya kufika nyumbani kwa marehemu alibaini kuwa vitu vilivyoungua ni pamoja na Bata,Sungura ,Kuku ,samani za ndani na fedha tasilimu .
Aliongeza kuwa marehemu baada ya kuzuka kwa moto huo akiwa ndani ya nyumba alifanikiwa kutoka nje yeye na familia yake lakini baada ya muda alikumbuka kuna fedha zake zipo ndani ndipo aliporejea kuzichukua ,hata hivyo alishindwa kutoka baada ya kuzingira na moto na kukosa njia ya kutoka ndani jambo lililopelekea kifo chake.
Alisema kuwa kikosi cha wokozi na zima moto kutoka mjini Arusha, walifika eneo la tukio na kukuta moto umeteketeza kila kitu ingawa wananchi hao walifanikiwa kumwokoa mke wa marehemu na mtoto ambao wanaendelea vizuri.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha marehemu katika hospitali ya mkoa Mount Meru na taratibu za maziko zinatarajiwa kufanyika siku leo siku ya jumatatu.
Kamanda wa polisi mkoani hapa,Justine Masejo hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo,jitihada zaidi za kumtafuta ili kuthibitisha tukio hilo zinaendelea.
Ends..
0 Comments