Watu wanne wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia ndani ya nyumba yao katika Kitongoji cha Kibumbe wilayani Rungwe, huku miili ikiwa imeharibika.
Watu hao ambao ni mume Simon Mtambo (41), mke wa Fortunata George (38) na watoto wawili, Oscar Mtambo (14) na Florence Mtambo (9) wanadaiwa wamepoteza uhai ndani ya wiki moja na kwamba chanzo cha kifo chao bado hakijafahamika.
Akizungumza baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk Vincent Anney, alisema tukio hilo ni moja kati ya mfululizo wa matukio ya mauaji na kujiua yanayotokea wilayani humo.
“Inasikitisha sana kifo cha baba, mama na watoto, tumeruhusu miili yao izikwe kwa sababu imeharibika. Nawaomba wananchi mnapokuwa na mgogoro hakikisheni mnatoa taarifa kwa mamlaka husika ili tuushughulikie,” alisema.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, katika wiki moja kati ya watu wanne hadi watano wanaripotiwa kuuawa au kujiua katika wilaya hiyo.
Hali hiyo, alisema imeilazimu Serikali kuona haja ya kufanya utafiti wa kujua sababu za kutokea kwa matukio hayo.
Alionya tabia za baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi wakiwaua wengine kwa dhana kuwa ni washirikina na kuwa Serikali itachukua hatua dhidi yao.
Diwani wa Kata ya Kiwira, Michael Mwamwembe alisema taarifa ya tukio hilo aliipata baada ya kupigiwa simu na polisi na alipofika katika nyumba hiyo alikuta miili imeharibika.
“Kwa wiki hii hili ni tukio la pili. Kuna mwanamke alimuuwa mumewe katika Kitongoji cha Mpandapanda na kisha kumfukia nje ya nyuma yake, sababu ni migogoro ya wivu wa mapenzi,” alisema.
Mfululizo wa matukio ya mauaji ya mapenzi, alisema yanaonyesha haja ya kutungwa sheria ndogo itakayoruhusu wanandoa kutengana iwapo watakuwa na migogoro, ili kunusuru uhai wao.
Ukimya wa wiki moja ndio uliomfanya mmoja wa ndugu kufunga safari kutoka Mbeya hadi nyumbani hapo, alisema mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina litajwe.
Alisimulia kuwa nyumbani hapo alikuta milango imefungwa, huku kukiwa na harufu kali, hali ambayo ilisababisha kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi.
Baada ya milango ya nyumba hiyo kuvunjwa, ndipo walikuta miili hiyo ya watu wanne.
“Tulipoingia ndani tulikuta hali hiyo, chini kulikuwa na panga na nyundo pamoja na paketi ya kuhifadhia dawa ya kuulia wadudu wa mbogamboga,” alisema.
Mkazi wa Kiwira, Ally Mwakipesile aliwataka wazee wa kimila kuingilia kati matukio hayo, akisema wanapaswa kukemea ili kuinusuru nguvu kazi.
Mwanamume alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Mbuja na mke mwalimu wa Shule ya Msingi Ikuti wakati mtoto mmoja alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Busokelo na mwingine shule ya msingi Ikuti.
0 Comments