Na Joseph Ngilisho Arusha
Naibu waziri ofisi ya makamu wa rais muungano na Mazingira ,Hamis Hamza Hamis ametoa miezi miwili kwa kiwanda cha kuzalisha vyandarua na Nguo cha A to Z kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha, kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kuchakata maji taka kutoka kuwandani hapo ili kuepusha malalamiko ya wananchi.
Akizungumza katika ziara aliyoifanya kiwandani hapo jana, mbele ya wataalamu wa mazingira kutoka Jiji la Arusha, Halmashauri ya Arusha na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC.
Naibu Waziri alisema kuwa ameridhishwa na hatua ya iliyofikiwa kwa mradi huo wa kuchakata maji taka na kukitaka kiwanda hicho kuhakikisha unakamilika ndani ya miezi miwili.
Alisema amefurahi kuona agizo ambalo serikali ililitoa kwa kiwanda hicho kuhusu kuongeza ukubwa wa mtambo wa kuchakata maji taka kiwandani hapo limetekelezwa na kwamba hivi sasa maji yatakuwa salama zaidi tofauti na hapo awali.
"Kwa namna nilivyopata taarifa na baada ya kufika hapa nimeona vitu viwili tofauti, nilijua nakuja kufunga kiwanda lakini imekuwa tofauti, hongereni sana AtoZ kwa kujali mazingira na afya za watu, lakini pia nimefurahi kwamba mnawapa wafanyakazi wenu maziwa hongereni sana, sasa nataka kujua huu mradi utakamilika lini," alipongeza na kuhoji.
Akijibu swali hilo Mkurugenzi Uzalishaji kiwandani hapo Binesh Haria amesema mtambo huo ambao umegharimu zaidi ya Bilioni1 umeshafikia hatua ya asilimia 95 kukamilika na kwamba baada ya miezi miwili utakuwa umekamilika kabisa na kuanza kutumika.
"Mheshimiwa Waziri,hadi Disemba tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa miradi huu na kuanza kutumika lakini hadi sasa umeshaanza majaribio, tunachokiomba ni serikali kuongea na mamlaka ya maji safi na taka Arusha (Auwsa), waweze kukamilisha bomba la maji taka ili na sisi tuweze kuunganisha maji yetu sababu hilo ndio lengo kuu,"alisema.
Kufuatia ahadi hiyo ya kukamilika kwa ujenzi huo, Naibu Waziri aliwaagiza maofisa wa mazingira katika Halmashauri za Arusha, Jiji na Nemc kushirikiana na kiwanda cha Atoz kuhakikisha mradi huo unakamilika vizuri na kuanza kufanya kazi huku akitoa wito kwa Auwsa kukamilisha kwa wakati bomba la maji taka linalokuja kiwandani hapo.
Alisema kiwanda cha Atoz ni miongoni mwa viwanda vikubwa ukanda wa Afrika na vimekuwa vikichangia pato kubwa kwa Serikali ikiwemo kutoa ajira nyingi kwa vijana na wanawake hivyo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaujali na kuthamini mchango wake.
Hata hivyo alisema pamoja na mchango huo, bado afya za wananchi wanaozunguka viwanda kama hivyo ni muhimu kuzingatiwa na ndio sababu kila mara serikali imekuwa ikifanya ukaguzi.
Katika hatua nyingine naibu waziri amekitaka kiwanda hicho kuzidisha huduma kwa wananchi wanaokizunguka kiwanda hicho ili kuimarisha mahusiano na ujirani mwema ,kwani kipato cha kiwanda hicho hakiendani na huduma wanazochangia kwa wananchi.
Naye meneja uzalishaji Mhandisi Harison Rwehumbiza alisema hadi sasa ujenzi wa mtambo huo umefikia asilimia 80 na sasa wanasubiri mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Auwsa kuunganisha bomba kubwa la maji taka na baada ya miezi miwili utakua umekamilika.
Ends...
0 Comments