Na Joseph Ngilisho, Arumeru
Wakazi zaidi ya 70 katika kata za Ngarananyuki , Ngabob na Uwiro,wilaya Arumeru Mkoani Arusha, kila wiki wananufaika na huduma bora za afya,uchunguzi ,ushauri ,elimu na tiba inayotolewa katika Kliniki ya Afrika Amini Alama iliyopo katika kitongoji cha Momela wilayani humo.
Akiongea na waandishi wa habari waliotembelea Kliniki hiyo ,inayotoa huduma za kitaalamu na tiba asili ,mganga mkuu ,Dkt Baraka Barati alisema Kliniki hiyo imeanza kutoa huduma za afya tangu Juni mwaka huu na imewafikia wakazi zaidi ya 3000 kwa gharama nafuu.
Alisema Kliniki hiyo inatibu magonjwa ya Kisukari,Presha, Saratani ya Mlango wa Kizazi,Tezi Dume, na Vidonda sugu vya Tumbo.
Huduma zingine ni pamoja na uchunguzi wa kimaabara ,Utrasound,uchunguzi wa Saratani ,huduma za macho ,ushauri na vipimo vingine.
Alisema kuwa Kliniki hiyo imejengwa maeneo ya vijijini ili kuweza kuwahudumia wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufuata matibabu mbali na makazi yao.
"Tumejiwekea utaratibu wa kila wiki kwenda kutoa huduma ya matibabu katika vitongoni mbalimbali na kila wiki tunawafikia watu 60 hadi 70 ambao tunawatia tiba,ushauri na elimu "alisema
Naye meneja uendeshaji wa Kliniki hiyo, Mohamed Abbas
alisema kuwa Kliniki hiyo iliyopo chini ya shirika lisilokuwa la kiserikali la Afrika Amini Alama,pamoja na kutoa huduma za afya linashirikiana na serikali katika nyanja za elimu ikiwemo kufadhili wanafunzi.
Alisema lengo la kuanzisha huduma hizo ni kusaidia wananchi wà kipato cha chini kwa kuwapatia huduma ya gharama nafuu au bure.
Alisema shirika hilo kupitia Kliniki hiyo lina program ya kuwahudumia wagonjwa waliopo majumbani kwa kuwafuata kijijini nakuwapatia huduma ya vipimo na wale wanaobainika kuwa na shida kubwa wanafikishwa katika Kliniki hiyo kwa ajili ya huduma zaidi.
"Tumeamua kufikisha huduma hii katika maeneo ya vijijini ili kuwasaidia kupata huduma kwa gharama nafuu au bure na kuepushe gharama kubwa ya kufuata huduma za afya"alisema
Kwa upande wake muuguzi wa kitengo cha Tiba asili ,Faraja Joseph alisema kuwa kitengo chake kinatoa huduma kupitia mashine ya kitaalmu inayochunguza mfumo wa mwili .
Alisema mashine inayojulikana kwa jina la Vitatec inachunguza kiwango cha Msongo wa mawazo ,kiwango cha sumu mwilini,kupima kongosho na ini na baadaye yeye kama mtaalamu hutoa ushauri na tiba ya dawa asili.
Awali mkurugenzi wa shirika hilo dkt Cornelia Wallner alisema lengo la kuanzisha kitengo cha tiba asili katika Kliniki hiyo ni kutoa fursa kwa wagonjwa walioathiliwa na kiwango cha sumu mwilini kupatia tiba ya dawa za asili ili kuondoa sumu mwilini.
Alisema Kliniki hiyo inahudumia wakazi mbalimbali katika mikoa ya kanda ya kaskazini ,aliwashauri watanzania kuwa na utaratibu wa kupima afya zao kwani wagonjwa wengi wanaofika katika Kliniki hiyo wanakuwa katika hali mbaya jambo ambalo linakuwa gumu kuwahudumia .
Baadhi ya wagonjwa waliofika katika Kiliniki hiyo Kanangila Nko na Zachary Ndewario walishukuru uwepo wa Kliniki hiyo kijijini hapo kwani imewasaidia kupata huduma bora ya afya na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma hiyo umbali mrefu.
Ends
.
0 Comments