BY NGILISHO NEWS, Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati nchini Tanzania, January Makamba amesema gharama halisi ya kuunganisha huduma ya umeme kwenye nyumba kwa wakazi wa mijini na vijijini ni Sh800,000.
Hata hivyo, amesema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ili kupunguza gharama hiyo kwa kutambua umuhimu wake na maisha halisi ya Watanzania.
Akizungumza jana kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, Makamba amesema fedha hizo zinazotumika kuongezea ili Watanzania wapate huduma hiyo ingeweza kutumika katika kuboreshea huduma zingine ikiwemo kupanua mtandao wa umeme.
“Mwananchi akitakiwa kulipa Sh 27,000 ajue Serikali inachangia Sh773,000 kutoka kwenye mfuko wake na tukisema mteja alipe Sh321,000 kwa kiwango hicho ajue Serikali inachangia Sh 489,000, ni muhimu lijulikane hili.
“Gharama halisi za umeme na kuunganishiwa ni bei ambazo zinawekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kwa hiyo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) haliwezi kutoza kiwango zaidi ya kilichopangwa na mamlaka husika,” amesema.
Waziri Makamba amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa Tanesco inaingia gharama kununua waya, mita na nguzo.
0 Comments