Na Joseph Ngilisho Arusha
Aliyekuwa Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dkt John Pima na wenzake watatu ,wameongezewa mashataka mengine mawili na kufikia sita badala ya mashtaka ya awali ambayo yalikuwa ni manne.
Baada ya kusoma mashtaka hayo upande wa Jamhuri ulidai kwamba wanatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake watatu.
Mbali na Dk Pima washtakiwa wengine ni aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha na uchumi, Mariam Mshana, aliyekuwa mkuu wa idara ya mipango na uchumi, Innocent Maduhu na Alex Daniel.
Kabla ya kusomea maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule aliomba kubadili hati ya mashtaka na kufanya hati hiyo kuwa na mashtaka sita badala ya manne ya awali.
Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, Wakili Janeth aliieleza mahakama kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17, katika kesi hiyo.
Akiwasomea makosa hayo, Sekule alidai kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kati ya Aprili 14 hadi 16,mwaka huu wakiwa waajiriwa wa Serikali kwa pamoja na kwa nia ovu walifanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kwa matumizi yao binafsi Sh,milioni 65 iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya matumizi ya umma.
Alitaja shitaka la pili ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri kinyume na sheria ambapo wanadaiwa Aprili 14,2022 walimdanganya mwajiri kupitia nyaraka yenye dokezo lililokuwa linahusiana na shughuli za kila siku za mwajiri ambapo walidanganya Daniel amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh,milioni 65 huku wakijua kwa kufanya hivyo ni kumdanganywa mwajiri.
Alidai shitaka la tatu ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri ambapo, Aprili 14, 2022 wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu, ikiwa na maelezo ya uongo yakionyesha Daniel amesambaza moramu kwa ajili ya matengenezo ya barabara na anadai Sh milioni 65 huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.
Shitaka la nne ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu kupitia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari marejesho ya masurufu iliyoandikwa Aprili 26, 2022 iliyohusiana na shughuli za mwajiri.
Alidai nyaraka hiyo ilikuwa na maelezo ya udanganyifu kuwa Alex anafanya marejesho ya Sh milioni 65 ikiwa ni matumizi ya kusambaza moramu katika taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara huku wakijua kwa kufanya hivyo wanamdanganya mwajiri.
Wakili Janeth alitaja kosa la tano ni kughushi sahihi ambapo alidai kuwa watuhumiwa hao Aprili 28,2022 walighushi sahihi ya Noel Letara ikionyesha amesambaza vifusi kwenye baadhi ya barabara za jamii na maeneo ya taasisi za Serikali.
Alisema kosa la sita linalowakabili wote ni kughushi sahihi ambapo alidai kuwa watuhumiwa hao Aprili 28,2022 walighushi sahihi ya James Raphael, ikionyesha amesambaza vifusi kwenye baadhi ya barabara za jamii na maeneo ya taasisi za serikali.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 28,2022 kwa ajili kutajwa na kuanza kusikilizwa Oktoba 6, 2022.
Ends....
0 Comments