Na Joseph Ngilisho Arusha
WAZIRI wa Maji ,Jumaa Aweso amesema kuwa wizara yake imeanza kufanya tathimini ya wafanyakazi wake ili kuwaondoa watumishi wa mamlaka hiyo wasiowajibika kutatua changamoto za maji kwa wananchi.
Aidha ameagiza wakuu wa mabonde ya Maji hapa chini wasiotaka kutembelea maeneo yao ya kazi ili kuzuia uharibifu wa vyanzo vya Maji unaosababishwa na wananchi kuvamia vyanzo vya maji ,waondolewe.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo mapema Leo wakati akizindua mradi wa uondoaji wa mchanga kwenye mto Nduruma unaotekelezwa na bonde la mto pangani na baadaye kuongea na wananchi wa kata za Mbughuni na Shangharai Burka,wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Alisema kuwa wananchi wamekuwa wakihusika katika uharibifu wa vyanzo vya Maji lakini wakuu wa mabonde wamebaki kimya wakisubiri kufyeka mazao yao, ambayo yameoteshwa kwenye vyanzo vya Maji jambo ambalo alisema ni kinyume na utaratibu.
"Wakuu wa mabonde wamekuwa wakikaa ofisini kucheza na Laptop hawatembelei maeneo yao ya kazi wakisubiri kufyeka mazao yaliyooteshwa na wananchi kwenye vyanzo vya Maji ,muda wote walikuwa wapi" alihoji .
Alisema wakuu wa mabonde lazima wajue mipaka ya maeneo yao ya kazi na washirikiane na mamlaka zingine na kuwashirikisha wananchi kuwaelimisha kuliko kusubiri kufyeka mazao yao.
Waziri Aweso aliongeza kuwa serikali imetoa kiasi cha sh,milionin100 kutekelez mradi huo na aliahidi kuongeza kiasi kingine kama hicho ili kukamilisha mradi huo,pia ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa kata hizo mbili kwa ajili ya kujengea vivuko na kujenga mahusiano.
Awali mkurugenzi wa bonde la pangani,Mhandisi Segule Segule ,anayetekeleza mradi huo ,aliishukuru serikali kwa kutoa kiasi cha sh,milioni 100 ,ili kufanikisha mradi huo ambapo kwa kipindi kirefu MTO huo umekuwa ukisababisha adha kwa wananchi kuzingirwa na Maji.
Alisema kuwa watu zaidi ya 700 kila mwaka wamekuwa wakiathiriwa na Maji ya mto huo ambayo husambaa bila kufuata mkondo wake kutokana na kujaa mchanga wakati wa kipindi cha mvua za masika ,huku wakati wa kiangazi wananchi hao hukumbana na vumbi zito linalotokana na Maji hayo.
Diwani wa Kata ya Shangharai Burka John Eliau alisema kuwa wanawake zaidi ya 10 wa Kata hiyo wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka mitano kutokana na maji ya mtò huo kuvamia makazi yao na wengine kusombwa na maji wakati wakivuka mto huo kwenda kujifungua.
0 Comments