WANANCHI WAELIMISHWE NJIA SAHIHI ZA KUHIFADHI VYANZO VYA MAJI

 

Na Gift Mongi ,Moshi


Taasisi zinazohusika na usimamizi wa rasilimali ya maji ikiwemo mamlaka ya maji bonde la Pangani na Idara ya Mali Asili na Misitu zimetakiwa kutoka ofisini na kwenda kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira.


Akizungumza mbele ya waziri wa maji Mheshimiwa Jumaa Aweso, mbunge wa Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi alisema wataalamu wengi wamekuwa wakikaa ofisini badala ya kutoka na kukutana na watumia maji na wadau wake ili kujua kero zao na njia sahihi ya kuzitatua.

Alishauri, wakikutana na wananchi, watabaini njia ambazo zimekuwa zikiathiri vyanzo vya maji na hivyo kuwa rahisi kubuni mbinu mbadala za kudhibiti uharibifu.


"Yaani wanabaki ofisini badala ya kwenda kuwatembelea watumia maji ambao ndio waangalizi wa vyanzo vya maji. Ni lazima wakaelimishwe njia sahihi za uhifadhi mazingira" alisema Prof Ndakidemi.


Mbunge huyo alibainisha kwamba kumekuwa na ujangili wa ukataji holela wa miti ya asili kama Mikufi kwenye vyanzo vya maji. Kitendo hiki kisipochukuliwa hatua za kisheria kitaangamiza vizazi vyetu.


Kwa mujibu wa Prof Ndakidemi ni kwamba, wananchi wakipewa elimu wataweza kuwa ni walinzi wazuri kwani kwa sasa huenda wanafanya uharibifu bila wao wenyewe kujua kutokana na uelewa duni walio nao.


Kwa upande wake, waziri wa maji Mhe. Jumaa Aweso alisema watumishi waliopo kwenye idara mbalimbali ndani ya wizara hiyo wanatakiwa kubadilika na kuachana na kufanya kazi kimazoea.


"Ni lazima tubadilike tuachane na ile dhana ya kufanya kazi kimazoea. Ni vyema tutoke tukasikilize wananchi wana shida gani na tuone namna ambavyo tunaenda kuziletea ufumbuzi" alisema.


Alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi mbali mbali katika mkoa wa Kilimanjaro. Alisema, dhamira ya awamu ya sita ni kuhakikisha maji yanapatikana na kumaliza kero za muda mrefu. "Hili litakuwa endelevu ikiwa tutatunza vyanzo vya maji". Alisema Waziri.


"Nimeshuhudia miradi inavyokwenda  kwa mkoa niwapongeze ila muongeze kasi katika usimamizi wa miradi hii ili iweze kukamilika kwa wakati Kama ambavyo ni malengo ya serikali yetu" Alisema.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments