SABAYA NA WENZAKE BADO PAGUMU,MAWAKILI WAO WAZUA JAMBO MAHAKAMANI



BY NGILISHO NEWS Moshi. 

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne imeahirishwa hadi Agosti 29, 2022 huku upande wa utetezi wakitoa maombi mawili kwa upande wa mahakama.

Maombi hayo ni kumpa muda Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutoa kibali cha mahakama kuisikiza kesi hiyo au kuwaondoa washitakiwa hao mahakamani hadi upelelezi utakapokamilika.

Ombi hilo limewasilishwa leo Ijumaa Agosti 12, 2022 na wakili wa upande wa utetezi, Mosses Mahuna mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha ambaye ndiye anayeisikiliza kesi hiyo.

Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka saba ikiwemo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, matumizi mabaya ya ofisi pamoja na rushwa ya Sh30milioni kutoka kwa mfanyabishara wa Bomang'ombe, Alex Swai.

Washatakiwa wengine katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2022 ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.

"Juni mosi mwaka huu shauri hili lilipoletwa mahakamani upande wa mashitaka walitueleza upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya karibu kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hii lakini ilipoahirishwa mpaka Juni 7 walibadilisha kauli na kusema upelelezi haujakamilika, iweje ofisi hiyo hiyo ya DPP inatoa kauli tofauti," alisema

"Tunachojiuliza ni je? ni kweli upelelezi haujakamilika au ni mbinu za kuendelea kuwaweka washitakiwa maana sasa hivi ni miezi miwili tangu wameletwa hapa, tunataka kujua ni nini hicho kinachopelelezwa?na ni kwanini walikamatwa wakati upelelezi haujakamilika, ni kitu gani kinachomfanya DPP asitoe hicho kibali? kwasababu tangu kesi hii ianze kuchunguzwa sasa ni mwaka mmoja na miezi sita," alisema

"Tunachokiona hapa ni kwamba DPP anajificha nyuma ya kivuli cha mahakama ,hivyo tunaiomba mahakama hii kumpa muda DPP wa kutoa kibali cha kuipa mamlaka Mahakama kusikiliza kesi hii na endapo itashindwa ijiongeze kwenye kifungu cha 91 cha CPA cha kuiondoa shauri hili hapa mahakamani,"


Post a Comment

0 Comments