Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Arusha(RTO),Solomon Mwangamilo amewaonya vikali wamiliki wa magari watakaoshindwa kuyafikisha magari yao kituoni ili yaweze kukaguliwa na kusisitiza watachukua hatua za kuwanyang'anya leseni za usafirishaji sanjari na kuwafikisha mahakamani.
Mwangamilo ametoa kauli hiyo leo wakati akiongoza zoezi la ukaguzi wa magari ya wanafunzi ambalo limeanza leo nchi nzima na kutaraji kukamilika Agosti 13 mwaka huu.
Katika zoezi hilo RTO,Mwamgamilo alisema kuwa wataanza kukagua magari yote ya wanafunzi katika wilaya za Arusha,Arumeru,Monduli,Karatu, Longido na kisha Ngorongoro ambapo jumla ya magari takribani 400 yanataraji kukaguliwa.
Akiongoza zoezi la ukaguzi RTO Mwangamilo alisema kuwa endapo mmiliki yoyote wa gari la wanafunzi atakayeshindwa kulifikisha gari lake kukaguliwa atanyang'anywa leseni ya usafirishaji na kisha kufikishwa mahakamani.
"Natoa angalizo endapo mmiliki yoyote atakayeshindwa kulifikisha gari lake likaguliwe kituoni tutamchukulia hatua kali za kisheria"alisema Mwangamilo
Hatahivyo,alisisitiza kuwa zoezi la ukaguzi wa magari ya wanafunzi mkoani Arusha limelenga kuhakikisha magari yote yanayosafirisha wanafunzi yanakuwa katika viwango vya ubora ili kuepusha ajali za barabarani.
Alisema kuwa katika zoezi hilo watatoa vibali maalum baada ya kujiridhisha na ubora wa gari husika na katika ukaguzi huo utahusisha kila mfumo wa ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna mmiliki wa gari atarekebisha gari lake.
"Ukaguzi huu hautaingiliana na ratiba ya masomo ya wanafunzi hivyo wamiliki wa magari hatutarajii wawe na visingizio vya aina yoyote hili zoezi sio wito ni lazima kwa kuwa ni zoeI la nchi nzima"alisisitiza Mwangamilo.
Ends...
0 Comments