Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
Mwili wa mkongwe wa siasa nchini Hayati Augustino Lyatonga Mrema (77)ambaye alifariki jana alfajiri Agosti 21 katika hospitaliya Taifa Muhimbili,utasafirishwa siku ya Jumatano jioni kutoka jijini dar salaam kuelekea kijijini kwake Kiraracha Mkoani kilimanjaro .
Kwa mujibu wa Mke wa marehemu, Dorine Kimbi hayari Mrema atapumzishwa katika nyumba yake ya milele siku ya ALHAMIS pembeni mwa kaburi la Mkewe Rose Mrema aliyefariki septemba 2021.
Mrema anatarajiwa kuzikwa na maelfu ya watu ukizingatia kwamba alikuwa kipenzi cha watu hawa akina mama aliowatetea wasinyanyaswe na waume zao kwa kuwataka watoe taarifa polisi chapu wakipigwa.
Tujikumbushe walau kidogo historia ya nyota Mrema......
Usiku mwingine tena,mwamba umelala,daima tutaikumbuka mikutano yako na wananchi, mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa, khanga zilizokuwa zikitandikwa na akina mama ili utembee juu yake wakati ukipita mitaani na mambo mengine.
Kumbukumbu yangu nzuri ilikuwa Mwaka 1995 ulipofika Ubungo ukitokea Moshi na kukuta umati wa watu ukikusubiri, ukatandikiwa kanga toka Ubungo hadi Manzese, watu walisema usiwashe gari wao wataisukuma.
Umati wa watu pembeni ya barabara wakaingia barabarani kuisukuma gari na wamama wakatandika khanga chini ili upite juu yake hadi Manzese uliposimamishwa tena na umati wa watu wakitaka uendelee kupiga chenga kuelekea kufunga goli kwenye Uchaguzi mkuu wa Urais mwaka 1995.
Tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania ilikuwa haijawahi kuona mwanasiasa wa upinzani mwenye nguvu na ushawishi kama Augustino Lyatonga Mrema,pengine kidogo tulikuja kuona mafuriko ya Lowassa yakifanana na umati wako.
Mrema ulikuwa unatisha wakati huo kwa hoja zako jadidi zilizogusa Wananchi na kuungwa mkono,baada ya kuvuliwa nyadhifa zote pale Dodoma, na kabla hujajiunga na chama chochote,Nccr Mageuzi ndio kilikuwa chama cha kwanza cha upinzani chenye nguvu za hoja lakini lakini hakikuwa na wafuasi kabisa,nakumbuka kuna mikutano ya hadhara ilikuwa inafanya na wahudhuriaji walikuwa watu kumi tu,kwa wakati huo Nccr ilikuwa na ngome imara kule Kongowe, Dar es Salaam,angalau pale kongowe miaka hiyo ya 1993 na 1994 ilikuwa wakifanya mikutano wanapata washabiki kidogo, kwa hiyo kama kuna mkutano wa Nccr walitaka waandishi wa habari waende kongowe ambapo ndio palikuwa na vibe na picha nzuri za mkutano.
Baada ya Mwenyekiti wa Nccr Mageuzi, Daktari Mabere Marando, James Mbatia, Daktari Masumbuko Lamwai, Daktari Ringo Tenga aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama na Anthony Komu kwenda kumuomba Mh Mrema kujiunga na Nccr Mageuzi hali ikabadilika ghafla katika kukubalika kwa chama cha Nccr Mageuzi,Nccr Mageuzi ikaanza kukubalika kwa ushawishi na hoja nzito za Mh Augustino Lyatonga Mrema,Nccr Mageuzi ikavunja rekodi ya kuujaza uwanja wa Jangwani, Nccr Mageuzi wenyewe hawakutarajia kama Mrema alikuwa na watu wengi kiasi hicho,Wakati huo,miaka ya 1994 taifa lilikuwa na mafisadi lakini Ndugu Mrema hakupata ushirikiano kama ambao baadhi ya vyama kama Chadema na wanasiasa kama Mh Mbowe na Tundu Lissu wanavyopata hivi sasa.
Ndugu Mrema alikuwa anapinga ufisadi,kuna suala la mfanyabiashara Chavda ambaye alikuwa na kashfa ya mamilioni ya mashamba ya mkonge,kuna suala la Loliondo,Wakati ule kabla ya kuvuliwa uanachama wa CCM,Mh Mrema alionekana kero kwa wenzake ndani ya Chama na Serikali na nje ya serikali, je angendeleaje katika mazingira kama hayo? Ndugu Mrema alipinga Ufisadi,na alitaka ufisadi uwe historia,alitaka kurejesha nidhamu ndani ya serikali hasa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya ndani na hata alipopandishwa cheo na Rais Ali Hassan Mwinyi,awe Naibu Waziri Mkuu, lakini watu wakawa wanampiga vita waziwazi,ilikuwa haiwezekani kubaki ndani ya chama na Serikali,bora aende akawe mpinzani labda huko angeweza kuleta mabadiliko,hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya Mh Mrema kuomba kuvuliwa nyadhifa zote za chama na Serikali ili ajiunge na upinzani na hasa NCCR Mageuzi,"
-Nccr Mageuzi na Chadema wamgombania Ndugu Augustino Lyatonga Mrema.
Nccr Mageuzi walifunga safari hadi nyumbani kwa Mh Mrema,walipofika pale walikutana naye,aliwakaribisha vizuri wakafanya naye mazungumzo,aliwaambia mambo mawili makubwa; Mosi alitaka vyama vyote vya upinzani viungane na yeye ndiyo awe mgombea wa upinzani na la pili lilikuwa kutaka apewe Uenyekiti wa NCCR,kikao kikaisha Nccr Mageuzi wakaondoka na kwenda kujadiliana pale Leader's Club, Kinondoni, Mwenyekiti wa Nccr Mageuzi,Daktari Mabere Marando akakubali kuachia ngazi ili Mrema awe Mwenyekiti.
Dk. Tenga naye akajiuzulu Ukatibu Mkuu ili Daktari Marando achukue nafasi yake,Vijana watatu wa Nccr Mageuzi wakati huo Mtemelwa,Blasius Loloma, Kezia Makoyo, Lugiko Kamnyabale na Komu,wakapewa kazi ya kupeleka majibu ya barua ya maamuzi ya Nccr Mageuzi kwa Mh Augustino Lyatonga Mrema,Vijana hao walipofika nyumbani kwa Ndugu Augustino Lyatonga Mrema alipewa taarifa kwamba Edwin Mtei, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati huo, naye alikuwa ameenda kumuona Mrema kumwomba ajiunge na chama chake Cha Chadema.
Vijana wa Nccr Mageuzi walipewa jibu kwamba vyama vyote vya upinzani vinatakiwa kufunga safari hadi Moshi mkoani Kilimanjaro ambako ndiko Mh Augustino Lyatonga Mrema amepanga kutangaza atajiunga na chama gani, Nccr Mageuzi wakapata taarifa kuwa Mwenyekiti wa Chadema,Ndugu Mtei alimpa Mh Mrema ofa ya kuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, ilijulikana kuwa Waziri huyo wa zamani, Mh Mrema alikuwa na nguvu sana katika kanda ya ziwa lakini kwa namna yoyote ile ofa ya Nccr Mageuzi ya kumpa Uenyekiti Mh Mrema ilikuwa kubwa kuliko ofa ya ukatibu mwenezi aliyopewa CHADEMA,Timu ya Nccr Mageuzi ikaanza maandalizi ya kwenda Moshi kumpokea Ndugu Augustino Lyatonga Mrema katika chama chao akitokea CCM,ilikuwa ni mwezi Machi 1995 lakini sikumbuki tarehe,Wakati huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro alikuwa ni Omar Mahita ambaye baadaye alikuja kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP.
Hatimaye, Machi, 1995, Mrema alitangaza rasmi kujiunga na NCCR katika tukio lililotetemesha nchi. Mwenyewe, ananiambia, alikuwa "amewasha moto." Kwa siku tatu mfululizo tangu Mrema ajiunge na NCCR,Nccr Mageuzi walitoa kadi nyingi kwa wanachama wapya kuliko kawaida,maombi yalikuwa mengi kiasi kwamba toka asubuhi hadi jioni watu walijaa katika kila ofisi ya Nccr Mageuzi,viongozi wa Nccr Mageuzi walikuwa wakitoka ofisini wamechelewa sana,
Kwa maoni yangu,nadhani kilichotokea wakati ule kinaweza kisitokee tena,pengine Mh Edward Lowassa aliweza kuifikia rekodi ya Mh Mrema kwa asilimia themanini, nazifuatilia siasa za upinzani tangu vyama vingi viruhusiwe na sijaona mwanasiasa aliyependwa kuliko Ndugu Augustino Lyatonga Mrema, Niseme bila unafiki kwamba Mh Augustino Lyatonga Mrema ni sehemu ya upinzani hapa Tanzania, tutake au tusitake,bila yeye, upinzani usingefika hatua hii,hebu tujiulize leo, ni wana CCM wangapi waliowahi kushika wadhifa kama wa Mh Mrema na halafu wakahama na kujiunga upinzani!??
Pumzika kwa amani,Mwamba wa Upinzani nchini Tanzania,Ndugu Augustino Lyatonga Mrema,daima tutakukumbuka kwa yote yale uliyoyaasisi ndani ya CCM,ndani ya Serikali na ndani ya Upinzani.
0 Comments