Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameunda kamati maalumu itakayo shughulikia upatikanaji wa eneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika leseni ya utafiti wa makaa ya mawe lililoshikiliwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa muda mrefu.
Dkt. Kiruswa ameunda kamati hiyo baada ya kutembelea eneo linalomilikiwa kwa ubia kati ya NDC kwa asilimia 25 na Maganga Mtitu International (MMI) kwa asilimia 75 lililopo kijiji cha Katewaka wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Kiruswa ametoa wiki 5 kamati hiyo iwe imekamilisha zoezi la kutafuta namna bora ya kuwapatia eneo wachimbaji wadogo wa madini ya makaa ya mawe, shaba na dhabibu ambayo yapo katika eneo hilo.
Pia, Dkt. Kiruswa ameitaka kamati hiyo kuwaelimisha kuhusu kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kupatiwa leseni na mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uchimbaji.
"Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi watendaji wake kuwalea wachimbaji wadogo na kuhakikisha kila mahali penye madini tunatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," amesema Dkt. Kiruswa.
Kutokana na eneo hilo kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba na makaa ya mawe, Dkt. Kiruswa ameagiza iwepo orodha ya wanaotaka kuchimba madini husika yaliyopo katika eneo hilo.
Dkt. Kiruswa ameunda kamati maalumu inayohusisha mjumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Ludewa, Ofisi ya Mkurugenzi wa NDC, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ludewa na Kampuni ya MMI.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea mgodi wa uchimbaji Makaa ya Mawe unaomilikiwa na Kampuni ya Milcoal uliopo katika kijiji cha Liombo kata ya Misimabhalasi wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.
Naye, Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Milcoal, Binod Kumar amesema mgodi huo una hifadhi ya zaidi ya tani milioni 1.2 za makaa ya mawe na uhai wa maisha ya mgodi huo ni miaka 15.
0 Comments