BY NGILISHO NEWS, Babati.
Mkazi wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Hamis Ramadhan (74) anashikiiliwa na polisi kwa tuhuma za kumkata panga, Petro Akwesoo (34) baada ya kumnywesha mkojo akimdanganya kuwa ni pombe.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Limited Mhongela akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Agosti 17, 2022 amesema tuko hilo limetokea Jumatatu ya Agosti 15, 2022 Kijiji cha Sabolo Kata ya Dabil.
Mhongela amesema chanzo cha tukio hilo la kukatwa panga la shingo ni Ramadhan kudanganywa na kupewa mkojo ukiwa ndani ya chupa na Akwesoo aliyemwambia anywe kwani ni pombe.
“Ramadhan alipokea chupa hiyo na kuinywa akidhani ni pombe ambayo ni maarufu hapa Manyara inayotengenezwa Babati ila alipoinywa kidogo akabaini ni mkojo siyo pombe,” amesema Kaimu kamanda Mhongela.
Amesema Ramadhan baada ya kubaini hiyo siyo pombe ni mkojo aliokunywa, alighadhibika na kuchukua panga na kumjeruhi nalo Akwesoo shingoni.
“Hadi hivi sasa tunamshikilia Ramadhan yupo mahabusu ila majeruhi Akwesoo yupo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara, akiendelea na matibabu,” amesema Mhongela.
Naye Mkazi wa Kata ya Dabil, John Awet amesikitishwa na kitendo hicho cha wakazi hao kufanya vitendo hivyo vya kujeruhi na kumnywesha mkojo na kusababisha matatizo kwenye jamii.
“Haya sasa wamegawana majengo ya Serikali bila sababu yoyote, huyu yupo mahabusu na yule anatibiwa hospitali ila tunatarajia heri itatawala kwa wote,” amesema Awet.
0 Comments