Ngilisho News ARUSHA.
Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima, umeombwa kuwabadilishia mashtaka yasiyo na dhamana kwani mmoja wao anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilipanga kutaja kesi hiyo namba 5/2022 ambapo mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine ni John Maduhu (aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango ya uchumi) na Mariam Mshana (aliyekuwa Mkuu wa Isara ya Mipango na uchumi).
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa, mtuhumiwa wa tatu (Maduhu), aliomba upande wa mashtaka uwafikirie katika kesi hiyo ambayo haina dhamana kwa kuwabadilishia mashtaka kwani anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Mtuhumiwa huyo aliieleza mahakama kuwa ana tatizo la moyo kupanuka hivyo anahitaji mazingira yenye amani, hivyo wanaomba kubadilishwa mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.
Awali Wakili wa Serikali Charles Kagilwa, alieleza mahakama kuwa shauri hilo limepangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake haujakamilika.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kagilwa, alisema kwa sasa hana la kusema na kuwa watajitahidi kukamilisha upelelezi.
Kwa upande wake Mariam, alieleza mahakama kuwa wanajua kesi hiyo ambayo upelelezi wake haujakamilika ndiyo inawafanya waendelee kukaa mahabusu hivyo wanaomba mahakama iangalie wapate dhamana katika kesi zingine mbili zinazowakabili na waletwe katika kesi hii upelelezi ukishakamilika.
Alieleza mahakama hiyo kuwa, ana mtoto mdogo anayetambaa na kuwa kutokana na mkusanyiko wa magereza, mtu mwenye mtoto anayetambaa analazimika kumbeba muda wote.
Hakimu mkazi huyo alimweleza mtuhumiwa huyo kuwa kuna baadhi ya makosa suala la dhamana linaweza kuzungumzwa ila baadhi ya makosa dhamana yake ni changamoto na kuwa kwenye makosa ambayo hayana dhamana katika kesi hiyo hana la kusema zaidi ya kutoa rai kwa Jamhuri kuharakisha upelelezi.
Katika kesi hiyo watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa sita likiwomo kosa la utakatishaji fedha Sh103 milioni, ambapo wanadaiwa kujipatia fedha hizo huku wakijua ni zao la uhalifu la kosa la kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao.
Awali mahakama hiyo iliahirisha kesi zingine mbili za uhujumu uchumi zinazowakabili watuhumiwa hao na wenzao wawili, Nuru Ginana na Alex Daniel, kutokana na Wakili wa Serikali anayesikiliza shauri hilo kudaiwa kuwa ni mgonjwa.
Katika kesi hizo watuhumiwa hao walikuwa wakitetewa na mawakili Sabato Ngogo na Joshua Minja ambapo leo mashauri hayo yalipangwa kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.
Wakili Ngogo aliiomba mahakama tarehe itakayotajwa kwa washitakiwa hao waweze kusomewa maelezo hayo ya awali kwani ni mara ya pili shauri hilo linapangwa kwa ajili ya kuwasomea maelezo hayo ya awali ila hawajaweza kusomewa.
Hakimu huyo aliahirisha kesi zote tatu hadi Julai 28,2022.
0 Comments