HOTELI YA IMPALA KUPIGWA MNADA MUDA WOWOTE


Na Joseph Ngilisho Arusha 


Hotel ya Kitalii yenye hadhi ya nyota tano ya Impala Hotel iliyokuwa ikimilikiwa na Mfanyabiashara maarufu, marehemu Faustine Mrema ,ipo hatalini kupigwa mnada kwa amri ya mahakama baada ya kushindwa kulipa deni la dola za kimarekani ,549,731 zilizoamriwa na mahakama.

Hatua hiyo imekuja kufuatia wakala wa benki ya NBC ambao ndio wadai wa kiasi hicho cha fedha ,kampuni ya Locus Attorneys ya jijini Dar es salaam kuzungushia utepe katika hoteli hiyo na kuwaamuru walinzi waliokuwepo eneo hilo kuondoka.



Akiongea na gazeti hili Mkurugenzi wa kampuni hiyo,dkt Onesmo Kyauke alisema kuwa uamuzi wa kuweka utepe ni hatua za awali za kuishikilia hoteli hiyo kama njia moja wapo ya kushinikiza kilipwa deni hilo.

Kyauke ambaye alijitambulisha kama mshirika mwenza wa benki ya NBC alisema ,baada ya siku 21 iwapo mdaiwa ambaye ni kampuni ya Impala Hotel atashindwa kulipa deni hilo,  benki itatangaza kuipiga mnada hoteli hiyo.

"Tumezungushia utepe hotel hii baada ya mdaiwa kushindwa kulipa deni aliloamuriwa na mahakama  na kuanzia leo tunatoa siku 21 iwapo kama mdaiwa anajitokeza aweze kulipa vinginevyo tutatangaza kuuza"alisema.

Hata hivyo  moja ya mawakili wa Benki ya NBC ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa alisema kuwa mahakama kuu kanda ya Arusha kupitia kesi ya madai namba 19/2019 ilimwamuru mdaiwa kulipa kiasi hicho cha fedha ndani ya siku 40 kuanzia siku ya hukumu Mei,19,2022 jambo ambalo halikufanyika.

Alisema kutokana na mdaiwa kukaa kimya na kushindwa kulipa deni hilo benki hiyo imeamua kushikilia hoteli hiyo kama hatua moja wapo ya kupata haki yao .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa hoteli ya Impala,Randy Mrema ambaye ni mtoto wa marehemu alisema ameshitushwa na hatua hiyo kwani suala hilo lipo ngazi ya mahakama ya rufaa na waliweka zuio.

Alisema ameshangazwa kuona benki ikizungushia utepe hoteli yao wakati suala hilo wameshalikatia rufaa kupinga hukumu ya mahakama kuu .

"Kilichofanyika ni uhuni na ukiukwaji wa sheria kwani hakuna amri ya mahakama ya kushikilia hoteli , tumekata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama kuu "alisema

Hata hivyo alisema kuwa pamoja na changamoto za kifamilia zinazopelekea kutofikia mwafaka wa kulipa deni hilo,alisema anampango wa kwenda mahakamani kulalamikia kitendo kinachoendelea na watadai fidia ya kuwadhalikisha.

Wakili wa benki ya NBC alikiri kupata kusudio la rufaa lakini alisema hakuna zuio inayowabana kutekeleza uuzwaji wa hoteli hiyo.

Ends..




















Post a Comment

0 Comments